UHISPANIA-CATALONIA-SIASA

Serikali ya Uhispania yatupilia mbali masharti ya Catalonia

Uhispania haitakubali masharti yoyote kutoka Catalonia, serikali ya Madrid imesema, huku ikibaini kwamba inataka kuendelea na mazungumzo na Barcelona kutatua mgogoro kuhusu eneo hilo kuwa taifa huru.

Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez.
Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez. REUTERS/Susana Vera
Matangazo ya kibiashara

Quim Torra, kiongozi wa serikali ya Catalonia, awali alisisitiza na kumuomba Waziri Mkuu Pedro Sanchez kufungua njia kwa mchakato wa kujitawala kwa Jimbo lake akimtishia kulishawishi bunge la kitaifa kutoendelea kumuunga mkono.

"Hatukubali masharti yoyote, kujitawala ndiyo, lakini uhuru kwa eneo la Catalonia hapana," amejibu Isabel Celaa, msemaji wa serikali kuu ya Uhispania.

Mvutano kati ya viongozi wa Catalonia na serikali kuu ya Madrid unaendelea kwa miezi kadhaa sasa, baada ya viongozi wa zamani kutimuliwa na kufunguliwa mashitaka ya kuchochewa uasi kabla ya mashitaka hayo kufutwa.