Baada ya Macron, Merkel atetea uundwaji wa jeshi la Ulaya
Imechapishwa:
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekuwa wa kwanza kujitokeza na kumuunga mkono Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, akitetea uundwaji wa jeshi la pamoja la Ulaya, jambo ambalo Rais wa Marekani Donald Trump ameendelea kupinga vikali.
Akilihotubia Bunge la Ulaya mjini Strasbourg kuhusu mtazamo wake kwa hatima ya Ulaya, Angela Merkel ametoa wito wa "kuweka fikra pamoja itakayoezesha kufika siku moja Ulaya inakuwa na jeshi moja lenye nguvu". Wabunge kutoka kambi yake ya mrengo wa kulia ya EPP wamekaribisha kauli hiyo na kutupiliwa mbali na wabunge kutoka kambi ya upinzani.
Msimamo huu unatolewa katika mazingira ya mvutano mkali kati ya Ufaransa na Marekanikuhusu suala hili. Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump ameendelea kukosoa pendekezo la Emmanuel Macron la kuunda kikosi cha jeshi la Ulaya kwa kukabiliana na vitisho vya Urusi na China.
Hata hivyo Kansela wa Ujerumani amejaribu kuonya wakosoaji wa msimamo huo, akisema: "Sio jeshi linalokuja kupinga shughuli za NATO, naomba nieleweke vizuri."
Pendekezo la kuunda jeshi la pamoja la Ulaya lilloanza kutolewa na raisa wa Ufaransa Emmanuel Macron tayari limezua sintofahamu kati ya Ufaransa na Marekani.