UINGEREZA-EU-MAY

May: Mkataba tuliokubaliana na Umoja wa Ulaya ni mzuri

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May AFP

Viongozi wa Mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya, watakutana siku ya Jumapili jijini Brussels nchini Ubelgiji, kujadili na kupitisha makubaliano yaliyoafikiwa kati ya Uingereza na wakuu wa Baraza hilo kuhusu ushirikiano utakaokuwepo, baada ya Uingereza kujiondoa mwezi Machi mwaka 2019.

Matangazo ya kibiashara

Makubaliano hayo yamewakasirisha wabunge nchini Uingereza ambao wengi wamesema hawakubaliani nao na wanamtaka Waziri Mkuu Theresa May, kufanya mazungumzo mapya.

Hata hivyo, May kwa mara nyingine amesema, makubaliano hayo ni mazuri kwa ajili ya maendeleo ya Ungereza na ushirikiano wake wa siku zijazo na mataifa mengine ya bara Ulaya.

Naye, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amesema atapinga mkataba huo iwapo suala la kisiwa cha Gibraltar hakitashughulikiwa. Kisiwa hicho kinamilikiwa na Uingereza lakini kipo katika eneo la Uhispania.

Naye rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk, amesema, makubaliano hayo, yanagusia namna Uingereza inatakavyoshirikiana na EU kuhusu masuala ya biashara, usalama, mazingira miongoni mwa mambo mengine.

Kuna uwezekano mkubwa wa wabunge nchini Uingereza, kuukata mkataba huo hata iwapo utapitishwa na wakuu wa mataifa mengine ya bara Ulaya.

Hii inamaana kuwa, kuna hatari ya Uingereza kuondoka EU, bila ya mkataba wowote wa ushirikiano.