UFARANSA-MAANDAMANO-USALAMA-UCHUMI

Rais wa Ufaransa achukua baadhi ya hatua kukabiliana na maandamano

Emmanuel Macron ahutubia taifa kutoka ikulu ya Elysée Desemba 10, 2018.
Emmanuel Macron ahutubia taifa kutoka ikulu ya Elysée Desemba 10, 2018. Olivier MORIN / AFP

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amelihutubia taifa wakati taifa hilo linaenelea kukumbwa na maandamano ya wanaharakati wanaopinga kuongezwa kwa kodi ya mafuta.

Matangazo ya kibiashara

Hotuba hiyo ya Rais Macron ya dakika kumi na tatu ilikua inasubiriwa kwa hamu na gamu wakati mgogoro wa "vizibao vya njano" umeendelea kushika kwa majuma kadhaa. Waandamanaji wenye hasira wamekua wakiomba kuchukuliwa hatua kali na thabiti katika nyanja mbalimbali kwa miaka kadhaa.

Rais Emmanuel Macron ameshtumu machafuko yaliyoibuka wakati wa mandamano hayo na kusema kuwa ni jambo lisilo kubalika ambalo limesababisha "hasara kubwa kwa nchi".

Pia amewanyooshea kidole cha lawama "viongozi wa kisiasa ambao malengo yao" ilikuwa ni kuzua vurugu na kusababisha machafuko nchini.

"Wakati kunazuka uhasama, uhuru unakuwa hatarini," amesema Emmanuel Macron akionya waandamanaji.

"Sijasahau kwamba kuna watu wenye hasira. Sitaki kuambatanisha hasira hiyo kwa tabia zisizokubalika ambazo nimezitaja, " ameongeza rais wa Ufaransa.

"Hiyo hasira, ninahisi tu kwa njia nyingi, inaweza kuwa ni njia chanya kwetu," amesema. "Hali inayowakumba haikuanza jana," lakini "tuliishi kwa kuzowea hali hiyo hadi kufikia hata kuisahau." "Ni miaka 40 tukiisha katika hali ngumu," rais Macron amesema, akishtumu watangulizi wake. Hata hivyo amesema anahusika kwa njia moja ama nyingine kwa hali hiyo.

"Inawezekana kuwa imetokea kwa bahati mbaya nikawaumiza baadhi ya watu kwa kauli mbali mbali "

Emmanuel Macron ametangaza "hali ya dharura ya kiuchumi na kijamii", hukua kisema kuwa anataka "kuingilia kati haraka".

Rais Macron amechukua baadhi ya hatua ili kukabiliana na maandamano yanayoendelea.

"Ninaomba serikali na Bunge kufanya kiliyo chini ya uwezo wao ili tuweze kuishi katika mazingira bora zaidi kuanzia mwanzoni mwa mwaka ujao.

Rais Macro ametangaza mshahara wa chini wa euro 100 kwa mwezi: "Mshahara wa mfanyakazi wa Smic utaongezeka kwa euro 100 kwa mwezi kuanzia mwaka 2019 bila hata gharama ya euro moja kwa mwajiri".

Pia amechukua hatua iliyowekwa chini ya utawala wa Nicolas Sarkozy na kufutwa chini ya utawala wa François Hollande: muda wa ziada utalipwa bila kodi au gharama kuanzia mwaka 2019, "bila hata hivyo kampuni kupoteza chochote".

Tangu maandamano hayo yalipoanza wiki tatu zilizopita, machafuko yameongezeka kwa kasi kila kunapoteokea maandamano katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris, ambako kulitokea machafuko makubwa siku ya Jumamosi wiki mbili zilizopita.

Kufuatia kuzuka kwa mgogoro uliosababishwa na waandamaji wanaopinga kuongezwa kwa kodi ya mafuta nchini Ufaransa, serikali imesema iko tayari kuachana moja kwa moja na hatua ya kupandisha kodi ya bidhaa hiyo kama hakutapatikana "ufumbuzi mzuri."