May: Kura mpya ya maoni itapoteza imani ya Waingereza
Imechapishwa:
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May anatarajia Jumatatu wiki hii kulihutubia bunge kuhusu upinzani wake dhidi ya kura ya maoni kuhusu Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya.
Theresa May amesema kura hiyo inaweza kusababisha wananchi "kutokuwa na imani tena na serikali" na kusababisha "uharibifu mkubwa".
Mapema wiki iliyopita Theresa May alitangaza kuahirishwa kwa zoezi la kusahihishwa makubaliano na Umoja wa Ulaya katika bunge, kwa hofu ya kukataliwa, na aliponea siku ya Jumatano kwa kura ya kutokuwa na imani naye kwa wabunge wa chama cha Consevative.
Wakati huo huo wanasiasa mbalimbalki wametoa wito wa kufanyika kwa kura mpya ya maoni ili kuondokana mgogoro wa kisiasa unaoendelea.
Hata hivyo serikali ya Theresa May imefutilia mbali hoja hiyo, ikisema itazidisha mgawanyiko na kukiuka uamuzi wa wananchi wa Uingereza ambao walipiga kura ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya mwaka 2016.
Hii itaongeza hatari kwa mchakato wa Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya bila makubaliano ikiwa imesalia miezi minne kabla ya kufikia tarehe mwisho ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya (Machi 29, 2019 siku).
"Tusipoteze imani ya Waingereza katika kujaribu kupanga kura mpya ya maoni," Theresa May amewaambia wabunge kulingana na muhtasari wa hotuba yake iliyotolewa siku ya Jumapili usiku.
"Kura mpya ya maoni itasababisha uharibifu mkubwa kwa sera zetu, kwa kuwa itawaambia mamilioni ya wananchi wa Uingereza ambao wanaamini demokrasia kuwa demokrasia hii haifanyi kazi."