UINGEREZA-MAY-AJIUZULU-SIASA

Waziri Mkuu Theresa May athibitisha kujiuzulu

Waziri Mkuu wa Uingereza  Theresa May akitangaza kujiuzulu wadhifa huo Mei 24 2019
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May akitangaza kujiuzulu wadhifa huo Mei 24 2019 REUTERS/Toby Melville

Theresa May ametangaza kuwa atajiuzulu kama Waziri Mkuu wa Uingereza tarehe 7 mwezi Juni, na kuachana na uongozi wa chama cha Conservative.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza kwa hisia nyingi, katika Ofisi ya Waziri Mkuu jijini London, May amesema kwa muda aliokuwa madarakani, alifanya alivyoweza kutekeleza maoni ya wananchi wa Uingereza, waliamua kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya mwaka 2016.

Aidha, amesema anaondoka kwa masikitiko makubwa kwa sababu ameshindwa kutekeleza ahadi aliyokuwa ameitoa kwa wananchi wa Uingereza kuwa atawaongoza kujiondoa kwenye Umoja huo kama walivyoamua.

Hadi kufikia tarehe 7 mwezi Juni, May ataendelea kuwa Waziri Mkuu wakati huu chama cha Conservative kikitafakari ni nani atakuwa kiongozi wa chama hicho na baadaye Waziri Mkuu.

Kiongozi wa upinzani bugeni Jeremy Corbyn, amesema uamuzi wa Theresa May kujiuzulu ni sahihi, kwa sababu amekubali kile ambacho nchi imekuwa ikitaka kwa miezi kadhaa sasa.

“Hawezi kuongoza na hawezi kukileta pamoja chama chake kilichogawanyika. Yeyote atakayekuwa Waziri Mkuu mpya, lazima aamue mustakabali wa nchi yetu kwa kuitisha Uchaguzi Mkuu mpya,” ameandika kupitia ukurasa wake wa Twitter.

May alikuwa Waziri Mkuu wa pili mwanamke, na amekuwa madarakani kwa miaka mitatu, baada ya kujizulu kwa mtangulizi wake David Cameron.

Harakati zake kuongoza Uingereza nje ya Umoja wa Ulaya, zilikwama mara tatu baada ya wabunge kukataa kuunga mkono mapendekezo yake.

Kabla ya uteuzi huo, alihudumu kwa miaka sita kama Waziri wa Mambo ya ndani.