EU-UFARANSA

Uchaguzi Ulaya: Vyama vyenye misimamo vyatawala matokeo

Chama cha Front Nationale kinachoongozwa na mwanamama Marine Le Pen kimemaliza katika nafasi ya kwanza kwenye uchaguzi wa umoja wa Ulaya nchini Ufaransa, matokeo ambayo ni pigo kwa utawala wa rais Emmanuel Macron anatetea umoja wa Ulaya.

Kiongozi wa vuguvugu la Ressemblement Nationale, Marine Le Pen, akihutubia wafuasi wake baada ya ushindi 26 Mei 2019
Kiongozi wa vuguvugu la Ressemblement Nationale, Marine Le Pen, akihutubia wafuasi wake baada ya ushindi 26 Mei 2019 Bertrand GUAY / AFP
Matangazo ya kibiashara

Chama cha Le Pen National Rally kimepata asilimia 23.31ya kura zote huku chama cha mrengo wa kati cha Emmanuel Macron kikipata asilimia 22.41 ya kura zote.

Makundi yote mawili yanatarajiwa kuwa na idadi sawa ya viti katika bunge la Ulaya na hii ni kutokana na Uingereza kutarajiwa kujitoa kwenye umoja huo.

Le Pen ambaye alishindwa vibaya katika uchaguzi uliopita dhidi ya rais Macron, ametoa wito kwa mkuu huyo wa nchi kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mkuu, pendekezo ambalo lilikataliwa haraka na Serikali.

“Ni uamuzi wa rais kuhitimisha hoja, yeye ambaye aliweka rehani utawala wake katika uchaguzi huu kwa kuufanya kama kura ya maoni kupitia sera zake,” alisema Le Pen katika hotuba yake ya mwishoni mwa juma.

Licha ya kuonekana kupata mafanikio kwenye uchaguzi huu, chama chake pia kimepoteza mashina mengi ya wananchi waliokuwa wakikiunga mkono ikiwa ni mara ya kwanza kupoteza tangu mwaka 2014 ambapo kilipata asilimia 24.9.

Katika majibu yao ya awali, washirika wa karibu wa rais Macron walisema wanaheshimu matokeo hatua ambayo imethibitisha kuwa upande wao umekubali kushindwa.

Mshauri wa rais Macron ambaye hakutaka jina lake lifahamike amesema hakutakuwa na mabadiliko katika Serikali na hii itamaanisha kuwa rais atahakikisha mabadiliko aliyoahidi yanatekelezwa ikiwemo kupunguza kodi kwa watu wa kipato cha kati na ile sera ya mafao.

Waziri mkuu Edouard Philippe amesema matokeo haya yamethibitisha mabadiliko makubwa katika siasa za Ufaransa na hasa kutokana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 ambapo vyama vya asili vilizidiwa na vuguvugu la rais Macron.