UMOJA WA ULAYA

Viongozi wa EU wanakutana Brussels baada ya uchaguzi

Viongozi wa umoja wa Ulaya wanaelekea mjini Brussels Ubelgiji kutathmini kilichotokea baada ya uchaguzi mkuu wa wabunge ikiwemo mjadala wa kutafuta watu watakaoziba nafasi za viongozi wanaomaliza muda wao.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa na kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakati walipokutana mwezi Machi mwaka huu nchini Romania.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa na kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakati walipokutana mwezi Machi mwaka huu nchini Romania. Ludovic Marin/Pool via REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Katika suala la kuziba nafasi imo nafasi ya mkuu wa tume ya Ulaya, Jean-Claude Juncker ambaye uteuzi wake unatarajiwa kudumu kwa miezi kadhaa kabla ya kuondoka.

Nchi ya Uingereza licha ya kuwa iko katika mchakato wa kujitoa kwenye umoja huo, pia inashiriki kwenye mazungumzo ya Brussels.

Kwa mara ya kwanza umoja wa Ulaya unashuhudia vyama vya mrengo wa kati vikiwa havina umiliki wa jumla katika bunge ambapo uchaguzi wa juma hili umeshudia vyama vya kimazingira na vile vyenye misimamo mikali na vile vinavyotaka mabadiliko vikiibuka na ushindi.

Matokeo haya yamezidisha sintofahamu zaidi ndani ya umoja wa Ulaya na ndio maana ni muhimu kwa viongozi hawa kukutana kujadili vizuri mustakabali ujao wa umoja huo.

Mazungumzo ya Jumanne ya wiki hii hata hivyo yanaweza yasitoke na majina ya watu wanaoweza kuziba nafasi za wale wanaoondoka.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May atahudhuria kikao hichi na watu wa karibu wa umoja wa Ulaya wanasema hakutakuwa na mazungumzo yoyote kuhusu mchakato wa nchi hiyo kujitoa.

Baadhi ya nafasi nyingine za juu zinazotarajiwa kuzibwa ni pamoja na ile ya Rais wa Baraza la umoja wa Ulaya inayokaliwa na Donald Tusk, mkuu wa benki ya Ulaya inayokaliwa na Mario Draghi pamoja na ile ya mkuu wa sera za kigeni inayokaliwa na Federica Mogherini.