IRAN-MAREKANI

Zarif: Hatuna mpango wa kumiliki silaha za nyuklia, aionya Marekani

Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif ameijibu Serikali ya Marekani baada ya rais Donald Trump kudai kuwa nchi yake haina nia ya kushinikizo mabadiliko ya kiutawala nchini Iran, badala yake inataka utawala wa Tehran uachane na urutubishaji wa nyuklia.

Picha kutoka maktaba ikimuonesha waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif.
Picha kutoka maktaba ikimuonesha waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif. REUTERS/David Mdzinarishvili
Matangazo ya kibiashara

Kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Zarif amesema Iran haina mpango wa kuwa na silaha za nyuklia na kuituhumu Marekani kwa kuendelea kuongeza wanajeshi kwenye eneo la mashariki ya kati hali inayozidisha sintofahamu zaidi kwenye ukanda.

Kiongozi wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei alishawahi kusma kuwa nchi yake haina mpango wowote wa kuwa na silaha za nyuklia, ambapo alitoa makataa ya kuhakikisha hakuna utengenezaji wa silaha hizo, alinukuliwa Zarif.

Matamshi yake yamekuja baada ya Jumatatu ya wiki hii rais Trump akiwa nchini Japan, kudai kuwa Marekani inataka kuhakikisha kunapatikana makubaliano mazuri ya mpango wa nyuklia wa Iran na sio vinginevyo.

Rais Donald Trump alivyoingia madarakani alitangaza kuitoa nchi yake katika mkataba wa nyuklia wa Iran uliotiwa saini na mataifa 6 yenye nguvu duniani, ambapo akatangaza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya utawala wa Tehrani.

Lakini tangu juma lililopita Marekani ilianza kutuma meli zake za kivita pamoja na wanajeshi zaidi kwenye eneo la mashariki ya kati kwa kile utawala wa Washington unasema inataka kukomesha hatari ya nchi ya Iran kwa nchi washirika za ukanda.

Mwezi Octoba mwaka jana rais wa Iran, Hassan Rouhani alidai kuwa utawala wa Marekani unafanya njama kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko ya utawala tuhuma ambazo sasa rais Trump anakanusha.

Viongozi wa Tehran hata hivyo licha ya vikwazo na vitisho vya Marekani na nchi washirika, wameendelea kusisitiza kutotetereka huku wakitoa wito kwa mataifa ya ulaya ambayo yamesalia kwenye mkataba uliopo kuilinda nchi yake.

Mwezi uliopita Iran ilitishia kujitoa kwenye mkataba huo na kuanza upya urutubishaji wa Urani ikiwa nchi za Ulaya hazitasimama kidete kuhakikisha mkataba uliopo unatekelezwa.