UINGEREZA-SIASA

Waziri mkuu mpya wa Uingereza kutangazwa Jumanne hii

Boris Johnson na Jeremy Hunt, wagombea ambao mmoja wao anatarajia kumrithi Theresa May kama waziri mkuu mpya wa Uingereza, wakati wa mjadala wa televisheni, Manchester Julai 9, 2019.
Boris Johnson na Jeremy Hunt, wagombea ambao mmoja wao anatarajia kumrithi Theresa May kama waziri mkuu mpya wa Uingereza, wakati wa mjadala wa televisheni, Manchester Julai 9, 2019. Matt Frost / ITV / AFP

Mwanasiasa wa Uingereza na Meya wa zamani wa London, Boris Johnson Jumanne wiki hii anatarajiwa kutangazwa kuwa waziri mkuu mpya ambaye atakuwa na jukumu la kuhakikisha nchi hiyo inajitoa kwenye Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31.

Matangazo ya kibiashara

Johnson ambaye katika kampeni zake ameapa kuhakikisha nchi hiyo inatoka ikiwa na mkataba au bila ya mkataba, anatarajiwa kukumbana na changamoto kubwa katika utekelezaji wa azma yake ikiwemo suala la Iran.

Licha ya kuwa Boris Johson anatarajiwa kushinda kiurahisi nafasi hiyo, anakabiliwa na upinzani kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Jeremy Hunt, ambaye licha ya kutoonekana kupewa nafasi, lakini ana uungwaji mkono wa wabunge wengi.

Suala la uamuzi wa nani atakuwa waziri mkuu ajae wa Uingereza sasa limebaki mikononi mwa Tory ambao leo wataamua ikiwa watamkabidhi kijiti Boris Johnson au kubadili karata zao na kumkabidhi kijiti Jeremy Hunt kuchukua nafasi ya Theresa May aliyejiuzulu.