UFARANSA-MAANDAMANO-USALAMA

Ufaransa kukumbwa na mamndamano makubwa

Makabiliano wakati wa maandamano, Paris Juni 16, 2020.
Makabiliano wakati wa maandamano, Paris Juni 16, 2020. REUTERS

Ufaransa inatarajia kushuhudia maamndamano makubwa kati ya wale walioruhusiwa na wale waliopigwa marufuku kuandamana Jumamosi hii Juni 20, 2020.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano yaliyobatizwa kwa jina la "Black Lives Matters" yanaendelea katika nchi mbalimbali duniani, ikiwa ni pamoja na nchini Ufaransa ambapo maandamano makubwa yanatarajiwa Jumamosi hii, Juni 20.

Maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi na mienendo isiyofaa ya polisi imeshuhudiwa katika wiki chache zilizopita. Jumamosi hii, maandamano yatafanyika katika miji mbalimbali kudai wahamiaji waharamu walioko nchini humo wapewe vitambulisho vya kuishi , na kutoa heshima zao kwa George Floyd, Mmarekani mweusi aliyefariki dunia akiwa mikononi mwa polisi.

Manispaa ya jijila Paris imeamua kuruhusu maandamano ya wale wanaodai wahamiaji waharamu walioko nchini humo wapewe vitambulisho vya kuishi. Maandamano hayo yataanza saa nane mchana (saa za Ufaransa) kwenye eneo la Taifa na kwenda hadi Stalingrad.

Maandamano mengine yaliyoruhusiwa na mamlaka, ni yale ya kutoa heshima ya mwisho kwa Lamine Dieng, Mfaransa mwenye asili ya Senegal aliyefariki dunia mwaka 2007 akiwa na miaka 25 baada ya kukamatwa na polisi jijini Paris. Maandamano hayo yamepangwa kufanyika katika eneo la Jamhuri.

Lakini maandamano yaliyoitishwa na jamii ya watu wa Chechen Jumamosi hii mchana yamepigwa marufuku baada ya makabiliano makali wiki hii kati ya watu kutoka jamii hii na wakaazi wa wilaya ya Dijon.

Maandamano mengine yaliyopigwa marufuku ni yale yaliyopangwa kufanyika karibu na Ubalozi wa Marekani yaliyoitishwa na shirika la haki za watu weusi kutoka Afrika kwa kumkumbuka George Floyd. Mamlaka imesema kuwa wana hofu kuwa maandamano hayo yanaweza kusababisha machafuko nchini.