UFARANSA-SIASA

Baraza jipya la mawaziri latangazwa Ufaransa

Uteuzi wa Castex, mwanasiasa wa upinzani anayeegemea siasa za mrengo wa kati, umewashangaza wengi ambao hawakutarajia rais Macron angefanya uteuzi huo.
Uteuzi wa Castex, mwanasiasa wa upinzani anayeegemea siasa za mrengo wa kati, umewashangaza wengi ambao hawakutarajia rais Macron angefanya uteuzi huo. REUTERS/Benoit Tessier

Baraza jipya la mawaziri chini ya waziri mkuu wa Ufaransa  Jean Castex ,limetangazwa na sasa linatarajiwa kufanya  mkutano wa kwanza na rais Emmanuel Macron.

Matangazo ya kibiashara

Kuna sura mpya katika Baraza hilo, lakini Wawiri wa afya Olivier Véran, Florence Parly wa Ulinzi waliohudumu katika serikali iliyopita wameteuliwa tena katika nafasi hizo.

Baraza hili jipya linakuja baada ya Castex kuteuliwa katika nafasi hiyo wiki iliyopita, baada ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa zamani Edouard Philippe.

Mabadiliko haya katika serikali ambayo yalipendekezwa na Rais Emmanuel Macron ambaye alitangaza kwamba "timu mpya" itaundwa ili kufuata "njia mpya" ya kisiasa kwa sehemu ya mwisho ya muhula wake hadi uchaguzi wa urais wa mwaka 2022.

Mabadiliko hayo yalipangwa kabla ya kufanyika uchaguzi, kwani serikali ya Macron imekuwa ikikosolewa wakati wa janga la virusi vya Corona.

Mabadiliko hayo yalifanyika kufuatia uchaguzi wa manispaa wa Jumapili iliyopita, ambapo chama cha Kijani kilikishinda chama cha Macron katika miji mikubwa nchini humo.

Uteuzi wa Castex, mwanasiasa wa upinzani anayeegemea siasa za mrengo wa kati, umewashangaza wengi ambao hawakutarajia rais Macron angefanya uteuzi huo.

Castex kabla ya kuteuliwa katika nafasi hii ya juu nchini humo amekuwa akiongoza Kamati inayosimamia mapambano dhidi ya maambukizi ya Corona na kuoanekana kufanikiwa.

Wachambuzi wa siasa nchini Ufaransa wanasema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022, rais Macron ameanza maandalizi ya mapema kwa kumeua mwanasiasa wa upinzani kuwa Waziri Mkuu, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuchaguliwa tena.

Wakati alipopewa madarakani, Edouard Philippe, alionekana kupata umaarufu mkubwa kumpita rais Macron, licha ya serikali yake kushuhudia maandamano makubwa mwaka uliopita ya vizibao vya njano kupinga mageuzi ambayo walidai yanawapendelea matajiri.