EU-CORONA-AFYA

Nchi za EU zapingana kuhusu ukubwa wa jumla wa mpango wa kuinua uchumi

Angela Merkel, Emmanuel Macron na Charles Michel wanakutana mwanzoni mwa mkutano wa kwanza wa ana kwa ana wa EU tangu kuzuka kwa ugonjwa wa Corona , huko Brussels Julai 17, 2020.
Angela Merkel, Emmanuel Macron na Charles Michel wanakutana mwanzoni mwa mkutano wa kwanza wa ana kwa ana wa EU tangu kuzuka kwa ugonjwa wa Corona , huko Brussels Julai 17, 2020. Stephanie Lecocq/Pool via REUTERS

Viongozi wa Umoja Ulaya wanatarajia kujaribu leo Jumamosi, ikiwa ni siku ya pili ya mkutano wao wa ana kwa ana huko Brussels, kubadili msimamo wa kundi la mataifa tajiri ya kaskazini, yakiongozwa na Uholanzi na Austria, kufikia makubaliano ya mpango mkubwa wa kuinua uchumi wa umoja huo ulioharibiwa na janga la Corona.

Matangazo ya kibiashara

Ni mara ya kwanza katika kipindi cha miezi mitano, kwa sababu ya janga la Covid-19, viongozi wa nchi na Serikali - wote wakivaa barakoa ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa Covid-19- wanakutana ana kwa ana huko Brussels.

Hapo jana viongozi hao walibaini kwamba mpango huo ni muhimu kwa ajili ya kuuokoa uchumi ambao umeporomoka na kuongeza imani katika Umoja wa UIaya, ambao kwa miaka mingi umeyumba kutoka kwa mgogoro mmoja hadi mwingine.

Kundi la mataifa tajiri ya kaskazini yakiongozwa na Uholanzi yanasisitiza msimamo wao kuhusu upatikanaji wa mfuko wa kuufufua uchumi, huku likipata upinzani kutoka Ujerumani, Ufaransa, mataifa ya kusini Italia na Uhispania na mataifa ya Ulaya mashariki.

Wajumbe wamesema viongozi hao 27 wanapingana kuhusu ukubwa wa jumla wa mpango huo, mgawanyiko kati ya ruzuku na mikopo inayoweza kulipwa katika mfuko wa kuufufua uchumi na masharti ya kisheria yanayoambatanishwa.

"Tutajaribu kuanza tena mambo tofauti kuokoa mkutano huo" Jumamosi, chanzo cha kidiplomasia kimesema.

Uchumi wa nchi za Umoja wa Ulaya upo katika mdororo mkubwa na wakati hatua za dharura za kuuokoa kama vile mipango ya kipindi kifupi ikielekea kuisha, hali inaonekana kuwa mbaya.