UHISPANIA-HAKI

Mfalme wa zamani wa Uhispania atafutwa kwa udi na uvumba baada ya kutuhumiwa ufisadi

Mfalme wa zamani wa Uhispania Juan Carlos, Mei 4, 2019.
Mfalme wa zamani wa Uhispania Juan Carlos, Mei 4, 2019. REUTERS/Francois Lenoir

Vyombo vya habari nchini Uhispania vimeripoti duru tofauti kuhusu aliko mfalme wa zamani wa nchi hiyo Juan Carlos, baada ya tangazo lake la hivi majuzi kuwa alitazamia kuondoka nchini.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 anakabiliwa na tuhuma za ufisadi kufuatia kandarasi ya ujenzi wa reli iliyopewa nchi ya Saudi Arabia.

Tamko la kasri ya kifalme lililotolewa Jumatatu Agosti 3 lilinukulu barua ya Juan Carlos kwa mwanawe na mfalme wa sasa, Filipe, akisema kwamba anataka kumuwezesha mwanawe huyo kuongoza kwa salama licha ya hasira za umma juu ya masuala ya maisha yake binafsi.

Mfalme huyo aliyewahi kuwa mashuhuri sana nchini mwake na ambaye bado anatumia jina la Mfalme Mkuu, aliripotiwa kwamba tayari ameshaondoka Uhispania, ingawa vyombo vya habari vya huko havijasema alipokwendea.

Juan Carlos aliingia madarakani mwaka 1975 baada ya kifo cha Jenerali Francisco Franco na alikuwa akiheshimiwa sana kutokana na jukumu lake la kuiongoza Uhispania kutoka kwenye udikteta kueleka utawala wa kidemokrasia.

Hata hivyo, heshima yake ilianza kuporomoka baadaye kutokana na mkururo wa kashfa zilizomfanya astaafu mwaka 2014.