EU-ICC-MAREKANI-HAKI-UCHUNGUZI-USHIRIKIANO

Umoja wa Ulaya: Tuko bega kwa bega na ICC licha ya vikwazo vya Marekani

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Fatou Bensouda, Mei 3, 2018
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Fatou Bensouda, Mei 3, 2018 AFP

Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana 'bega kwa bega' na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, ICC, baada ya Marekani kutangaza vikwazo dhidi ya mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, Fatou Bensouda, msemaji wa Tume ya umoja huo amesema.

Matangazo ya kibiashara

Peter Stano amebaini kwamba Umoja wa Ulaya ulikuwa umeelezea msimamo wake wa kutokubaliana na Washington.

"Umoja wa Ulaya unapinga kabisa majaribio yote ya kudhoofisha au kupaka matope mfumo wa kimataifa wa haki kwa kukwamisha kazi ya taasisi zake kuu (...) ICC ni mmoja wa wahusika wakuu katika mapambano dhidi ya uhalifu, tuko bega kwa bega na ICC na hatujafurahishwa na hatua zilizochukuliwa dhidi ya shughuli zake ”, ameongeza Peter Stano wakati wa mkutano wa kila siku na waandishi wa habari.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alitangaza jana kuwa Marekani imeweka vikwazo dhidi ya mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC Fatou Bensouda kwa sababu ya ofisi yake kuendelea na uchunguzi wa watu wa Marekani.

Washington imeamua kumuweka mwendesha mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda, na pia mmoja wa washirika wake Phakiso Mochochoko kwenye orodha nyeusi. Vikwazo vya kiuchumi pia vimechukuliwa dhidi yao. Hatua ambazo zinaweza pia kuathiri mtu yeyote ambaye anashirikiana na mwendesha mashtaka, amesema Mike Pompeo.

Mahakama hiyo iliopo mjini Hague kwa sasa inachunguza iwapo vikosi vya Marekani vilifanya uhalifu nchini Afghanistan.

Marekani imeikosoa mahakama hiyo tangu ilipoanzishwa na ni miongoni mwa mataifa mengi ambayo hayajatia saini mkataba wa raia wake kushtakiwa na mahakama hiyo.