UINGEREZA-CORONA-AFYA

Rekodi ya kesi mpya yathibitishwa nchini Uingereza tangu Mei 30

Uwezo wa upimaji nchini Uingereza pia umeongezeka tangu kuripoti idadi kubwa ya maambukizi mwaka huu.
Uwezo wa upimaji nchini Uingereza pia umeongezeka tangu kuripoti idadi kubwa ya maambukizi mwaka huu. © Simon Jacobs

Uingereza imerekodi kesi mpya 1,940 za maambukizi ya virusi vya Corona, ikiwa ni rekodi tangu Mei 30, kulingana na takwimu za serikali ya nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Idadi ya kesi za kila siku imefikia 1,000 kwa siku kwa kipindi kikubwa cha mwezi wa Agosti, lakini kesi hizi zilijikuta zimeongezeka katika siku za hivi karibuni. Uwezo wa upimaji nchini Uingereza pia umeongezeka tangu kuripoti idadi kubwa ya maambukizi mwaka huu.

Hivi karibuni shirika la afya Duniani, WHO, lilizitaka nchi zote kutilia mkazo hatua za kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona na kuonya kuwa licha ya jitihada zinazofanyika kutafuta chanjo na dawa ya kupambana na janga la virusi vya Corona, huenda kusiwe na suluhu ya muda mrefu ya kukabiliana na janga hili.

Wakati huo huo Jarida la kila wiki la matibabu la Lancet limechapisha ripoti inayosema wagonjwa waliohusika katika majaribio ya awali ya chanjo ya Urusi ya virusi vya corona wameonyesha kupata kinga na wala hawakupata athari zozote mbaya kutokana na chanjo hiyo.

Hata hivyo wataalam wanasema watu waliofanyiwa majaribio walikuwa wachache mno kuthibitisha usalama wa chanjo hiyo.

Urusi ilitangaza mwezi uliopita kwamba chanjo yake kwa jina "Sputnik V" tayari imeidhinishwa. Suala ambalo liliibua hofu miongoni mwa wanasayansi wa Magharibi kuhusiana na chanjo hiyo kutokuwa salama.

Baadhi walionya kuwa kuharakisha kutafuta chanjo ni jambo la hatari. Urusi ilisema ukosoaji huo ni njama ya kuubeza utafiti wake.