Ufaransa yawekwa chini ya masharti mapya kukabiliana na maambukizi zaidi ya Corona
Imechapishwa:
Wakati nchi ya Ufaransa ikishuhudia ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, rais wa Ufaransa Emmanuel ametangaza makataa mapya ya watu kutotoka nje kuanzia usiku wa Jumamosi tangu saa Tatu Usiku hadi saa Kumi na Mbili asubuhi nchini mwake.
Akilihutubia taifa siku ya Jumatano rais Macron amesema kuwa amri hii ya kutotoka nje itahusu majimbo kadhaa likiwemo jimbo la Ile-de-France na katika miji mingine minane, na kuongeza kuwa Wafaransa watalazimika kuzoea kuishi na virusi "hadi msimu wa joto wa mwaka 2021.
Hivi karibuni Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean Castex alitoa wito kwa wananchi wa Ufaransa kuwa na "nyoyo za uwajibikaji" kwa kuvaa barakoa, jambo ambalo 'ni muhimu sana' katika mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa COVID-19.
Mlipuko wa virusi vya corona unaosababisha ugonjwa wa COVID-19, ulitokea katika mkoa wa Hubei nchini China mwishoni mwa mwaka 2019.
Kufikia sasa kinachojulikana ni kuwa COVID-19, ni ugonjwa ambao unaothiri mfumo wa kupumua wa binadamu.
Dalili zake ni pamoja na homa kali, kukohoa ambako baada ya wiki moja muathiriwa anakabiliwa na tatizo la kupumua.