Covid-19: Watu milioni 20 wawekwa chini ya makataa mapya nchini Ufaransa
Zuio la kutotoka nje limeanza kutumika Jumamosi hii usiku wa manane nchini Ufaransa: watu milioni 20 wamewekwa chini ya makata mapya katika majimbo mbalimbali ya Ufaransa ikiwa ni pamoja na Ile-de-France na katika miji mingine 8.
Imechapishwa:
Watu wamepigwa marufuku ya kutotembea kuanzia saa tatu usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi. Lengo ni kuvunja mkondo wa janga la Covid-19, ambalo linaendelea kuongezeka.
Ufaransa imeendelea kushuhudia ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.
Akilihutubia taifa siku ya Jumatano rais Macron alisema kuwa amri hii ya kutotoka nje itahusu majimbo kadhaa likiwemo jimbo la Ile-de-France na katika miji mingine minane, na kuongeza kuwa Wafaransa watalazimika kuzoea kuishi na virusi "hadi msimu wa joto wa mwaka 2021.
Hivi karibuni Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean Castex alitoa wito kwa wananchi wa Ufaransa kuwa na "nyoyo za uwajibikaji" kwa kuvaa barakoa, jambo ambalo 'ni muhimu sana' katika mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa COVID-19.
Mlipuko wa virusi vya corona unaosababisha ugonjwa wa COVID-19, ulitokea katika mkoa wa Hubei nchini China mwishoni mwa mwaka 2019.
Kufikia sasa kinachojulikana ni kuwa COVID-19, ni ugonjwa ambao unaothiri mfumo wa kupumua wa binadamu.
Dalili zake ni pamoja na homa kali, kukohoa ambako baada ya wiki moja muathiriwa anakabiliwa na tatizo la kupumua.