ITALIA-CORONA-AFYA

Italia: Conte kutangaza hatua mpya kuzuia kuenea kwa Corona

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte.
Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte. TIZIANA FABI / AFP

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte anatarajia kutangaza hatua mpya siku ya Jumapili kukabiliana na kuongezeka kwa maambukizi mapya ya Corona nchini humo, ofisi yake imesema.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa eneo la Liguria, iliyoko kaskazini mashariki mwa nchi, alikuwa ametangaza badala yake kuwa Roma inafikiria kuongeza masharti ya kuzuia raia kutembea wakati nchi hiyo siku ya Jumamosi iliripoti rekodi ya kila siku ya visa vipya vya ugonjwa wa Corona.

Giovanni Toti amesema Waziri wa Afya Roberto Speranza alikutana na Mamlaka Jumamosi kujadili hatua mpya zinazowezekana.

"Tunajadili kuhusu hatua zenyewe," Giovanni Toti ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, huku akiongeza kuwa serikali itazitaka shule na makampuni kuchukuwa hatua zaidi kukabiliana na maambukizi zaidi.

Italia, nchi kubwa barani Ulaya ambayo ilikuwa ya kwanza kuathiriwa na mlipuko wa Corona mwanzoni mwa mwaka huu, ilifanikiwa kudhibiti janga hilo wakati wa msimu wa joto baada ya kutekeleza vizuizi vikali vya jumla, lakini maambukizi yameongezeka sana katika wiki za hivi karibuni.

Siku ya Jumamosi, Wizara ya Afya ilitangaza kuwa watu wengine 10,925 waliambukizwa virusi vya Corona katika muda wa saa 24 zilizopita, rekodi mpya ya kila siku, na vifo 47 vilivyotokana na virusi.