UFARANSA-COVID19

Miji 8 ya Ufaransa yasalia mahame baada ya kuanza kutekelezwa kwa Curfew

Jiji la Paris likiwa tupu bila watu, saa chache baada ya kuanza kutekelezwa kwa makataa ya watu kutoka nje kuanzia saa 3 usiku hadi saa 12 asubuhi ili kudhibiti maambukizi ya Covid 19
Jiji la Paris likiwa tupu bila watu, saa chache baada ya kuanza kutekelezwa kwa makataa ya watu kutoka nje kuanzia saa 3 usiku hadi saa 12 asubuhi ili kudhibiti maambukizi ya Covid 19 THOMAS COEX / AFP

Mitaa ya jiji la Paris pamoja na miji mingine karibu 8, ilisalia mahame kuanzia hapo jana, saa chache tu baada ya kuanza kutekelezwa kwa makataa ya watu kutembea usiku. 

Matangazo ya kibiashara

Makataa haya yenye utata yaliyotangazwa na Serikali, yanalenga kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona ambavyo kwa majuma kadhaa taifa hilo limekuwa likirekodi ongezeko la juu. 

Wamiliki wa migahawa wamelalamikia makataa haya, ambayo wanasema yatasababisha warejee katika hali mbaya ya kiuchumi ambayo walishuhudia wakati wa makataa za awali. 

Hatua kama hizi zilizochukuliwa na Ufaransa, zinatarajiwa pia kuchukuliwa na mataifa kadhaa ya Ulaya, ikiwemo nchi ya Italia. 

Nchi ya Italia, ambayo ilikuwa ndilo taifa la kwanza kwenye ukanda huo kuathirika pakubwa na ugonjwa wa Covid 19, imerekodi maambukizi ya juu katika siku za usoni. 

Waziri mkuu wa Italia, Giuseppe Conte, anatarajiwa kutangaza makataa zaidi siku ya Jumapili, ili kudhibiti maambukizi zaidi. 

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa huenda makataa mpya zikalenga huduma zisizo za muhimu kama vile nyumba za mazoezi, mabwawa ya kuogelea na michezo isiyo ya lazima. 

Nchini Ufaransa, karibu watu milioni 20 wanakabiliwa na makataa haya mapya, ambapo watakaolazimika kusalia ndani ni pamoja na raia wa kwenye miji ya Marseille, Lyon, Lille na Toulouse pamoja na mji mkuu Paris, ambapo watalazimika kukaa ndani kuanzia 3  usiku hadi saa 12 asubuhi. 

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, anasema hatua hizi mpya zilizochukuliwa ni muhimu ikiwa nchi hiyo inataka kudhibiti kutokea kwa mlipuko mpya wa virusi vya Corona. 

Hata hivyo maelfu ya raia wa nchi hiyo wameeleza kuchukizwa nayo, wakisema itaathiria shughuli zao za kila siku hasa wafanyabiashara. 

Siku ya Jumamosi Ufaransa ilirekodi maambukizi mapya elfu 32 katika siku, ikizidi idadi iliyoripotiwa siku ya Ijumaa, ambapo watu zaidi ya elfu 26 walithibitishwa kuwa na maambukizi. 

Katika mataifa kadhaa ya Ulaya, ikiwemo nchi ya Slovakia, waziri mkuu Igor Matovic, amesema sasa serikali itapima watu wote wenye umri wa miaka 10 pamoja na wazee, wakati huu nchi hiyo ikirekodi idadi ya juu ya maambukizi. 

Serikali ilitangaza hali ya dharura mwanzoni mwa mwezi huu, ambapo ikatangaza makataa mapya ikiwemo kuzuiwa kwa ibada na shughuli nyingine zisizo za muhimu.