UFARANSA-USALAMA

Mwalimu aliyekatwa kichwa: Polisi yaendesha operesheni dhidi ya watu kadhaa

"Mimi ni mwalimu", huo ni ujumbe uliowekwa kwenye vipeperushi vilivyowekwa mbele ya chuo cha Bois d'Aulne, miongoni mwa shada za maua na mishumaa.
"Mimi ni mwalimu", huo ni ujumbe uliowekwa kwenye vipeperushi vilivyowekwa mbele ya chuo cha Bois d'Aulne, miongoni mwa shada za maua na mishumaa. REUTERS/Charles Platiau

Polisi nchini Ufaransa inaendesha operesheni kabambe tangu mapema Jumatatu asubuhi na operesheni hiyo itaendelea katika siku zijazo dhidi ya "watu kadhaa" kutoka makundi ya Kiislamu, Waziri wa Mambo ya Ndani ametangaza.

Matangazo ya kibiashara

Tangu kuuawa kwa Samuel Paty, mwalimu wa chuo cha Bois d'Aulne huko Conflans-Sainte-Honorine siku ya Ijumaa, chunguzi zaidi ya 80 pia zimefunguliwa kwa chuki kwa njia ya mtandaoni na watu kadhaa wamematwa, Waziri wa Mambo ya Ndani Gérald Darmanin ameongeza kwenye kituo cha Europe 1.

Hata hivyo Waziri Darmanin amesema kuwa anataka kufuta mashirika kadhaa yenye uhusiano na makundi yenye msimamo mkali wa kidini, ikiwa ni pamoja na muungano wa mashirika yanayodai kutetea Uislamu nchini Ufaransa (CCIF).

Hayo yanajiri wakati maelfu ya watu wameandamana nchini Ufaransa kuonyesha mshikamano dhidi ya kisa cha mwalimu aliyechinjwa kwa kuwaonyesha wanafunzi vibonzo vya Mtume Mohammed.

Kisa cha mwalimu huyo wa historia Samuel Paty kukatwa kichwa nje ya shule viungani mwa mji wa Paris Ijumaa iliyopita, kimeibua ghadhabu nchini Ufaransa na kukumbusha wimbi la machafuko ya Waislamu wenye itikadi kali ya mwaka 2015, ambayo pia yalichochewa na kuchapishwa kwa vibonzo vya Mtume Mohammed kwenye jarida la Charlie Hebdo.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alisema shambulio hili lina kila ishara ya uhusiano na masuala ya itikadi kali na ugaidi, na kwamba mwalimu huyo aliuawa kwa sababu tu ya kuwafundisha wanafunzi wake uhuru wa kujieleza.