UFARANSA-USALAMA

Propaganda za Kiislam mtandaoni, usalama katika shule: Paris yatangaza hatua muhimu

Baraza la Ulinzi lililoongozwa na Emmanuel Macron Jumapili jioni lilimemua kuimarisha usalama katika shule mwanzoni mwa mwaka wa shule na kuchukuwa haraka "hatua thabiti" dhidi ya propaganda za Kiislam zenye msumamo mkali mtandaoni, ikulu ya Elysee imesema.

Mbele ya chuo cha Bois d'Aulne huko Conflans-Sainte-Honorine, ambapo mwalimu aliyekatwa kichwa alikuwa akifundisha, Oktoba 16.
Mbele ya chuo cha Bois d'Aulne huko Conflans-Sainte-Honorine, ambapo mwalimu aliyekatwa kichwa alikuwa akifundisha, Oktoba 16. REUTERS/Charles Platiau
Matangazo ya kibiashara

Rais Macron "ametaka hatua za haraka zichukuliwe na kuwadhibiti wale wanaojipanga kupinga sheria za jamhuri", imeongeza Elysee, baada ya mkutano uliodumu saa 2 na 30 ambao mawaziri sita na mwendesha mashtaka dhidi ya ugaidi Jean-François Ricard wameshiriki.

Baraza limepanga kuimarisha usalama katika shule mwanzoni mwa mwaka wa shule Novemba 2, na hatua zitachukuliwa ndani ya wiki mbili.

Mawaziri wa Mambo ya Ndani na Sheria, Gérald Darmanin na Eric Dupond-Moretti, wamewasilisha "mpango wa utekelezaji ambao utatekelezwa wiki hii na ambao utaambatana na hatua dhidi ya hali hiyo, ikiwa ni pamoja na mashirika au watu walio na uhusiano wa karibu na makundi yenye misimamo mikali ya kidini”, ambayo yanaeneza jumbe za chuki ambazo zinaweza kuchochea mashambulizi, ofisi ya rais imesema.

Hayo ni baada ya mwalimu Samuel Paty kuuawa baada ya kukatwa kichwa kwa kuonesha wanafunzi vibonzo vya Mtume Muhammad.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alisema shambulio hili lina kila ishara ya uhusiano na masuala ya itikadi kali na ugaidi, na kwamba mwalimu huyo aliuawa kwa sababu tu ya kuwafundisha wanafunzi wake uhuru wa kujieleza. 

Mwendesha mashtaka wa Serikali, Jean-Francois Ricard, alimtaja mtuhumiwa kuwa ni Abdoulakh A mwenye umri wa miaka 18, aliyezaliwa mjini Moscow na mwenye asili ya watu wa Chechen.

Ricard, alisema mtuhumiwa aliingia nchini Ufaransa na kupewa kibali cha kuishi kama mkimbizi na alikuwa akifahamika na idara ya makachero waliokuwa wakimfuatilia.

Taarifa iliongeza kuwa, mtuhumiwa alienda chuoni hapo Ijumaa mchana na kuanza kuwauliza wanafunzi kuhusu mwalimu huyo. 

Baadae inadaiwa alimfuata mwalimu Paty aliyekuwa akirejea nyumbani kwa mguu, ambapo alianza kwa kumshambulia kichwani kwa kitu chenye ncha kali na kumjeruhi vibaya kabla ya kumchinja.