UFARANSA-USALAMA

Mauaji ya mwalimu Ufaransa: Watu 7 kufikishwa mbele ya jaji wa masuala dhidi ya ugaidi

Maafisa wa polisi wakikusanyika mbele ya chuo cha Bois d'Aulne huko Conflans-Saint-Honorine, kaskazini mwa jiji la Paris, baada ya mauaji ya mwalimu Samuel Paty, Oktoba 16, 2020.
Maafisa wa polisi wakikusanyika mbele ya chuo cha Bois d'Aulne huko Conflans-Saint-Honorine, kaskazini mwa jiji la Paris, baada ya mauaji ya mwalimu Samuel Paty, Oktoba 16, 2020. AP Photo/Michel Euler

Watu saba wakiwemo watoto wawili wanatarajia kufikishwa Jumatano hii mbele ya jaji wa kupambana na ugaidi kwa nia ya kufungua uchunguzi wa kimahakama na mashtaka baada ya mauaji ya mwalimu Samuel Paty siku ya Ijumaa karibu na mji wa Paris.

Matangazo ya kibiashara

Jumatano hii, Oktoba 21, watu watatoa heshima ya mwisho kwa mwalimu huyo huko Sorbonne. Katika kikao cha baraza la mawaziri, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitangaza kufutwa kwa muungano wa mashirika Cheikh Yassine.

Brahim C, ambaye mwanae alikuwa akifundishwa na mwalimu Samuel Paty ni miongoni mwa watu saba ambao wanatarajiwa kufikishwa mbele ya jaji wa kupambana na ugaidi kwa uwezekano wa mashtaka.

Brahim C. alizindua kampeni ya uhamasishaji dhidi ya mwalimu Samuel Paty baada ya kuwaonyesha wanafunzi vibonzo vya Mtume Mohammed katika shule yake ya Conflans-Sainte-Honorine, karibu kilomita ishirini kaskazini magharibi mwa Paris.

Wachunguzi wa kupambana na ugaidi wanajikita hasa na mazungumzo yaliyorushwa kwenye WhatsApp kati ya Brahim C. na mshambuliaji, Abdoullakh Anzorov, 18, mkimbizi mwenye asili ya Chechen.

Kwenye mkutano wa Baraza la Ulinzi, ulioongozwa na Rais Emmanuel Macron usiku wa kuamkia leo, iliamuliwa kwamba hatua kali zichukuliwe nchini humo dhidi ya itikadi kali na pia juhudi zaidi kuelekezwa dhidi ya matamshi ya chuki mitandaoni. 

Waziri wa mambo ya ndani amesema tangu kisa cha kuuawa kwa mwalimu huyo siku ya Ijumaa, takriban malalamiko 80 yamewasilishwa kuhusu chuki inayoenezwa mitandaoni inayokisifu kitendo hicho. 

Awali, mshukiwa mkuu wa uchinjaji huo mwenye umri wa miaka 18, alijigamba mitandaoni na kuandika kwamba mwalimu huyo alimdhalilisha Mtume Mohammed.