UFARANSA-USALAMA

Mauaji ya Samuel Paty: Macron atoa wito kwa umoja dhidi ya wanamgambo wa Kiislam

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakati wa hafla ya kitaifa ya kuuga mwili wa Samuel Paty, huko Sorbonne, Oktoba 21, 2020.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakati wa hafla ya kitaifa ya kuuga mwili wa Samuel Paty, huko Sorbonne, Oktoba 21, 2020. AP Photo/Francois Mori, Pool

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameongoza mamia ya waombolezaji kuuaga mwili wa Samuel Paty, mwalimu aliyekatwa shingo katika mazingira yenye kutatanisha jijini Paris.

Matangazo ya kibiashara

Rais Macron amesema ni mhanga wa ugaidi unaoendelea kukita mizizi nchini mwake kwa misingi ya kidini.

Haya yanajiri wakati mwendesha mashtaka wa kupambana na ugaidi nchini humo Jean-François Ricard akiyataja mauaji hayo kuwa tukio la kigaidi na kwamba watu saba wakiwemo watoto wawili, wanaendelea kushikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Brahim C, ambaye mwanae alikuwa akifundishwa na mwalimu Samuel Paty ni miongoni mwa watu saba ambao wanatarajiwa kufikishwa mbele ya jaji wa kupambana na ugaidi kwa uwezekano wa mashtaka.

Brahim C. alizindua kampeni ya uhamasishaji dhidi ya mwalimu Samuel Paty baada ya kuwaonyesha wanafunzi vibonzo vya Mtume Mohammed katika shule yake ya Conflans-Sainte-Honorine, karibu kilomita ishirini kaskazini magharibi mwa mji wa Paris.

Wachunguzi wa kupambana na ugaidi wanajikita hasa na mazungumzo yaliyorushwa kwenye WhatsApp kati ya Brahim C. na mshambuliaji, Abdoullakh Anzorov, 18, mkimbizi mwenye asili ya Chechen.

Kwenye mkutano wa Baraza la Ulinzi, ulioongozwa na Rais Emmanuel  Macron usiku wa kuamkia jana, iliamuliwa kwamba hatua kali zichukuliwe  nchini humo dhidi ya itikadi kali na pia juhudi zaidi kuelekezwa dhidi  ya matamshi ya chuki mitandaoni. 

Waziri wa mambo ya ndani amesema tangu kisa cha kuuawa kwa mwalimu  huyo siku ya Ijumaa, takriban malalamiko 80 yamewasilishwa kuhusu chuki  inayoenezwa mitandaoni inayokisifu kitendo hicho. 

Awali, mshukiwa mkuu wa uchinjaji huo mwenye umri wa miaka 18,  alijigamba mitandaoni na kuandika kwamba mwalimu huyo alimdhalilisha Mtume Mohammed.