UTURUKI-UFARANSA-USHIRIKIANO

Uturuki: Recep Tayyip Erdogan ahoji 'afya ya akili' ya Emmanuel Macron

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan huko Ankara, Oktoba 14, 2020.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan huko Ankara, Oktoba 14, 2020. Murat Cetinmuhurdar/Presidential Press Office/Handout via REUTE

Ofisi ya rais nchini Ufaransa imeshutumu matamshi ambayo yalionekana kuwa "hayakubaliki" yaliyotolewa na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye alihoji "afya ya akili" ya mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa sababu ya mtazamo wake kwa Waislamu na muswada wa sheria ya Ufaransa juu ya 'kujitenga'.

Matangazo ya kibiashara

Paris imelaani kile ilichokiita "matusi" na imetangaza kumrudisha nyumbani balozi wake jijini Ankara, mji mkuu wa Uturuki, kwa ajili ya mashauriano.

Mapema mwezi huu, Macron aliapa kupambana dhidi ya kile alichokiita kujitenga kwa wafuasi wa itikadi kali ya Uislamu, ambako alisema kunatishia kuchukua udhibiti wa baadhi ya jamii za Waislamu nchini Ufaransa, hatua iliyokaripiwa vikali na Erdogan.

Ufaransa ilighadhabishwa na kukatwa kichwa kwa mwalimu wa historia na mfuasi wa itikadi kali, aliyetafuta kulipiza kisasi kwa hatua ya mwalimu huyo kutumia vibonzo vya Mtume Muhammad katika darasa lake la uhuru wa kujieleza.

Rais wa Uturuki alisema Oktoba 6 baada ya matamshi ya kwanza ya Macron kuhusu "Uislamu wa kujitenga", kwamba matmshi hayo ni "uchokozi wa wazi" na yalionyesha ufidhuli wa kiongozi huyo wa Ufaransa.

Uturuki na Ufaransa ni wanachama wa jumuiya ya NATO lakini zimekuwa katika malumbano juu ya masuala kadhaa, yakiwemo sera nchini Syria na Libya, mipaka ya baharini mashariki mwa Mediterania na mzozo katika jimbo la Nagorno-Karabakh.

Erdogan ni Muislamu mcha Mungu na tangu chama chake cha AKP chenye misingi yake ya Kiislamu kuingia madarakani mwaka 2002, ametafuta kuufanya Uislamu kuwa sehemu ya siasa kuu nchini Uturuki, taifa lenye idadi kubwa sana ya Waislamu lakini lililokuwa linafuata misingi ya kilimwengu.