UTURUKI-UCHUMI

Uturuki: Gavana wa benki kuu afutwa kazi

Gavana wa benki kuu ya Uturuki Murat Uysal amefutwa kazi na nafasi yake kuchukuliwa na waziri wa zamani wa fedha Naci Agbal, kulingana na agizo la rais lililotolewa Jumamosi wakati sarafu ya Uturuki inaendelea kupteza thamani yake.

Gavana wa Benki Kuu ya Uturuki Murat Uysal huko Ankara, Julai 29, 2020.
Gavana wa Benki Kuu ya Uturuki Murat Uysal huko Ankara, Julai 29, 2020. AFP
Matangazo ya kibiashara

Bwana Uysal alichukuwa wadhifa huo mnamo mwezi wa Julai 2019 baada ya kufutwa kazi kwa mtangulizi wake, pia kwa agizo la rais.

Waziri wa Fedha kutoka mwaka 2015 hadi 2018, Bwana Agbal ameteuliwa kuwa gavana mpya na wa benki kuu ya taifa, na hakuna sababu iliyotolewa ya kuchukua nafasi hiyo ya Uysal.

Bwana Uysal alirithi wadhifa huo kufuatia utata kati ya gavana wa zamani, Murat Cetinkaya, na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan juu ya kupunguwa kwa viwango vya riba.

Rais Erdogan anapinga vikali kuongezeka kwa kiwango chochote cha riba, ambacho aliwahi kusema kuwa ni "mama na baba wa maovu yote."

Jumamosi iliyopita, rais Erdogan alitangaza kwamba Uturuki ilikuwa ikipambana na "pembetatu ya kishetani ya viwango vya riba, viwango vya ubadilishaji na mfumko wa bei".

Katika miezi ya hivi karibuni, sarafu ya Uturuki ilifikia viwango vya chini katika historia yake dhidi ya dola ya Marekani.

Sarafu ya Uturuki imepoteza karibu 30% ya thamani yake dhidi ya dola ya Marekani mwaka huu.

Masoko yana wasiwasi juu ya mfumuko wa bei unaoendelea, na kushuka kwa kasi kwa akiba ya fedha za kigeni.Mwezi uliopita, wengi walitarajia benki kuu ingeongeza kiwango kikubwa cha riba kufuatia kuchuka kwa thamani ya sarafu ya Uturuki, lakini masoko yalikatishwa tamaa wakati hakuan mabadiliko yaliyofanyika.

Benki ilishangaza wawekezaji mnamo mwezi wa Septemba wakati ilipandisha kiwango muhimu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2018, kutoka 8.25% hadi 10.25%.

Uamuzi unaofuata wa Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki juu ya viwango vya riba unatarajiwa kuchukuliwa mnamo Novemba 19.