ITALIA-CORONA-AFYA

Utafiti: Corona ilikuwa ikizunguka nchini Italia mnamo mwezi Septemba 2019

Mlipuko wa virusi vya Corona unaosababisha ugonjwa wa Covid-19, ulitokea katika mkoa wa Hubei nchini China mwishoni mwa mwaka 2019.
Mlipuko wa virusi vya Corona unaosababisha ugonjwa wa Covid-19, ulitokea katika mkoa wa Hubei nchini China mwishoni mwa mwaka 2019. NEXU Science Communication/via REUTERS

Virusi vya Corona vilikuwa vikizunguka nchini Italia mapema mwezi Septemba 2019, kulingana na utafiti uliofanywa na kituo cha kitaifa dhidi ya Saratani (INT) huko Milan, kikibaini kwamba virusi vya SARS-CoV-2 viliweza kuenea nje ya China mapema kuliko watu wanavyofikiria.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema virusi vya Corona na COVID-19, ugonjwa unaosababishwa na virusi hivyo, ulikuwa hajulikani kabla ya visa vya kwanza kuripotiwa mnamo mwezi Desemba mwaka jana huko Wuhan. katikati mwa China.

Walakini, WHO, ambayo inasema inachunguza utafiti wa INT, tayari imebaini kwamba "uwezekano kwamba virusi huenda vilisambaa mahali pengine bila kujulikana hauwezi kufutiliwa mbali".

Matokeo ya utafiti wa kituo cha kitaifa dhidi ya Saratani (INT) nchini Italia, uliyochapishwa na jarida la kisayansi la Tumori Journal of INT, yanaonyesha kuwa 11.6% ya watu 959 waliojitolea, wenye afya nzuri, walisajiliwa kama sehemu ya uchunguzi wa saratani ya mapafu kati ya mwezi Septemba 2019 na mwezi Machi 2020 walikuwa na kingamwili maalum dhidi ya virusi vya Corona kabla ya mwezi Februari.

Vipimo vingine kuhusu kingamwili dhidi ya SARS-CoV-2 vilifanywa na Chuo Kikuu cha Siena kama sehemu ya utafiti huo ulioitwa "ukaguzi usiyotarajiwa wa kingamwili dhidi ya SARS-CoV-2 katika kipindi cha kabla ya janga nchini Italia."

Hii inaonyesha kuwa kesi nne, zilizojitokeza wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba 2019, zilibeba kingamwili, Giovanni Apolone, mmoja wa waliofanya utafiti huo, ameliambia shirika la habari la REUTERS. Amebaini kwamba hii inamaanisha kuwa watu hao walikuwa wameambukizwa virusi vya Corona mnamo mwezi Septemba 2019.

"Hili ndilo hitimisho kuu: watu ambao hawakuonyesha dalili sio tu kuambukizwa baada ya vipimo vya serolojia, lakini pia walibeba kingamwili zenye uwezo wa kuua virusi," amesema."Hii inathibitisha kuwa virusi hivi vya Corona vinaweza kusambaa kati ya watu kwa muda mrefu na kusababisha kiwango kidogo cha vifo, na sio kwa sababu vinapotea, na vinajitokeza tena ghafla," ameongeza.

Watafiti wa Italia waligundua mnamo mwezi Machi idadi kubwa ya visa vya homa ya mapafu na mafua huko Lombardy katika robo ya nne ya 2019, jambo lingine ambalo linaweza kuthibitisha kuwa virusi vya Corona vilikuwa vikizunguka mapema zaidi kuliko ilivyozungumzwa hapo awali.