UINGEREZA-CORONA-AFYA

Watafiti: Chanjo ya Chuo Kikuu cha Oxford dhidi ya virusi vya Corona yatoa ulinzi wa asilimia 90

Mwanasayansi anayefanya utafiti kuhusu virusi vya Corona katika maabara ya Pfizer.
Mwanasayansi anayefanya utafiti kuhusu virusi vya Corona katika maabara ya Pfizer. REUTERS

Chanjo dhidi ya virusi vya Corona iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza, ina uwezo wa kuzuia watu kupata dalili za maambukizi ya virusi hivyo kwa kiasi kikubwa baada ya kumalizika kwa majaribio kuhusu uwezo wa chanjo hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Matokeo ya majaribio ya chanjo hiyo, yameonesha kuwa inatoa ulinzi wa asilimia 70 lakini watafiti wanaeleza kuwa ulinzi huo unaweza kuongezeka na kufikia asilimia 90.
Huu umeonekana kama ushindi kubwa kuelekea kupata chanjo ya Covid 19 baada ya kampuni ya Pfizer na Moderna nchini Marekani hivi karibuni kutangaza kuwa chanjo iliyogundulika inatoa ulinzi kwa asilimia 95.

Hata hivyo, chanjo ya Chuo Kikuu cha Oxford inaelezwa kuwa ya bei nafuu na rahisi kuhifadhi na hivyo kuwa rahisi kufika katika maeneo yote ya dunia.

Iwapo chanjo hiyo itathibitishwa na watalaam kuwa salama, itakuwa ni hatua kubwa ya kupiga vita maambukizi ya COVID-19 ambayo yameendelea kuisumbua dunia tangu mwishoni mwa mwaka 2019.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema kupatikana kwa chanjo hiyo ni habari njema wakati huu uthibitiho unaposubiriwa. Tayari serikali ya Uingereza imeagiza Dozi Milioni 100 ya chanjo hiyo kutoka Chuo Kikuu cha Oxford.