URUSI

Coronavirus: Urusi kutoa chanjo kwa zaidi ya wanajeshi 400,000

Urusi inapanga kutoa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa zaidi ya wanajeshi 400,000, Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu amesema leo Ijumaa.

Rais wa Urusi, Vladmir Putin.
Rais wa Urusi, Vladmir Putin. Kirill KUDRYAVTSEV / AFP
Matangazo ya kibiashara

Sergey Shoigu, akinukuliwa na mashirika ya habari ya Urusi, amesema wanajeshi 2,500 tayari walipewa chanjo dhidi ya COVID-19 na kwamba watafikia 80,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu.

 

Urusi ilikuwa nchi ya kwanza mnamo mwezi wa Agosti mwaka huu kuruhusu matumizi ya dawa, iliyopewa jina la Sputnik V, kwa chanjo dhidi ya COVID-19.

 

Katikati mwa mwezi Novemba, mbali na watu waliojitolea kwa majaribio ya kliniki, watu 10,000 waliotambuliwa kama watu walio katika hatari kubwa ya maambukizi, madaktari au walimu kwa mfano, walipewa chanjo.

 

Urusi inafanya majaribio ya kliniki ya dawa zingine (tofauti na dawa ya Sputnik V) kwa chanjo dhidi ya virusi vya ambavyo vimeua zaidi ya watu milioni 1.43 ulimwenguni tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

 

Alexandre Rijikov, mkurugenzi wa Taasisi ya Vector huko Siberia, ambayo inatengeneza dawa ya EpiVacCorona, amesema leo Ijumaa kuwa maabara yake iko tayari kutoa hadi dozi milioni 5 kwa mwaka.

 

Pamoja na maambukizi 2,215,533, Urusi ni nchi ya nne iliyoathirika zaidi ulimwenguni na janga la COVID-19 kwa idadi ya maambukizi nyuma ya Marekani, India na Brazil. Nchi hiyo imerekodi rasmi vifo 38,558 kutokana na COVID-19.