BREXIT-UINGEREZA-EU

BREXIT: Mambo bado magumu baina ya pande mbili

KUTOKA MAKTABA:Waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson akiwa na rais wa tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen.
KUTOKA MAKTABA:Waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson akiwa na rais wa tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen. Daniel LEAL-OLIVAS / AFP

Timu za majadiliano kutoka Serikali ya Uingereza na umoja wa Ulaya, wameendelea kukutana katika kile kinachoelezwa pengine ni siku mbili za mzisho za majadiliano ili kupata makubaliano kuhusu Brexit, baada ya kushindwa kukubaliana katika kipindi cha miezi 8.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa ujumbe wa EU, Michel Barnier na mwenzake wa Uingereza, David Frost, wameendelea kukutana jijini Brussels, baada ya siku ya Ijumaa kushindwa kukutana kutokana na kutofautiana pakubwa kuhusu masuala ya msingi ya mkataba wa Brexit.

Kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Barnier aliandika "Tutaona kama kutakuwa na uelekeo wowote".

Aidha waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, anaripotiwa kuwa atajaribu kuwashawishi viongozi wa Ulaya baada ya kuzungumza kwa simu na rais wa tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, ambapo pia walitofautiana pakubwa.

Viongozi hawa watajaribu tena kuzungumza kwa simu siku ya Jumatatu, kabla ya wakuu wa nchi za Ulaya kukutana Brussels, Alhamisi ya wiki ijao kujadili bajeti yao ya kunusuru uchumi kutokana na janga la Corona.

Mkutano huu licha ya kuwa utajadili mkwamo wa mapendekezo ya bajeti ya awali ambayo ilikataliwa na nchi kadhaa, suala la Uingereza kujitoa kwenye umoja wao linatarajiwa kugubika mkutano wao.

Licha ya kuwa masuala maengi wamekubaliana, viongozi hawa wanashindwa kufikia muafaka katika masuala ya haki za uvuvi, biashara sawa na kikosi kazi kitakachosimamia utekelezwaji wake.

Uingereza ilijitoa rasmi mwezi Januari baada ya miaka 4 tangu kufanyika kwa kura ya maoni, kura ambayo iliigawa nchi hiyo vipande viwili.