UFARANSA

Paris: Vurugu zashuhudiwa katika maandamano ya kupinga sheria ya usalama

Waandamanaji wakiwarushia vitu polisi jijini Paris, kupinga muswada wa sheria tata kuhusu usalama.
Waandamanaji wakiwarushia vitu polisi jijini Paris, kupinga muswada wa sheria tata kuhusu usalama. France24

Mamia ya waandamanaji nchini Ufaransa, wamekabiliana na polisi kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Paris, haya yakiwa ni maandamano mapya kupinga muswada wa sheria tata kuhusu usalama.

Matangazo ya kibiashara

Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi baada ya waandamanaji waliofunika nyuso zao kuanza kuvunja maduka na kuchoma moto magari kadhaa.

Zaidi ya maandamano 100 nchi nzima yalishuhudiwa hapo jana, raia wakipinga muswada wa sheria tata ambao utakataza watu kuwarekodi picha za video polisi wakati wakikabiliana na waandamanaji.

Wapinzani wa muswada huo wanasema utaminya uhuru wa vyombo vya habari na kuruhusu unyanyasaji wa polisi dhidi ya raia.

Nchi ya Ufaransa imekuwa ikishuhudia maandamano ya kila wiki kupinga muswada huo, maandamano yaliyoongezeka baada ya kuonekana kwa picha za video zikiwaonesha polisi wakimpiga kijana mmpja mwenye asili ya kiafrika ambaye ni mzalishaji wa muziki.

Hata hivyo kambi ya rais Emmanuel Macron, baada tu ya kuanza kwa maandamano haya, ilisema sehemu ya muswada huo utarekebishwa, lakini hata hivyo haijatosha kuwafanya waandamanaji kutojitokeza.

Siku ya Ijumaa rais Macron, alikiri kuwa "Kuna polisi ambao ni wanyanyasaji na inafaa waadhibiwe".

Maelfu ya waandamanaji wakiwemo wale wa vizibao vya njano waliokuwa wanaipinga Serikali walishiriki maandamano ya mwishoni mwa juma hili, ambapo baada ya kutokea kundi la waandamanaji waliofunika nyuso zao na kuanza kuharibu mali, ndipo polisi walilazimika kutumia nguvu kuwakabili waandamanaji.