VATICAN-IRAQ-ZIARA

Papa Francis kuzuru Iraq mwezi Machi, ziara ya kwanza ya kihistoria

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis Filippo MONTEFORTE / AFP

Kiongozi wa Kanisa katoliki anatarajia kuzuru nchi ya Iraq Machi 5 hadi 8, ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuanza kwa janga la COVID-19. Hii itakuwa ziara ya kwanza ya kihistoria kwa kiongozi huyu wa Kanisa, Holy See imetangaza leo Jumatatu.

Matangazo ya kibiashara

"Akikaribisha mwaliko wa Jamhuri ya Iraq na Kanisa Katoliki, Papa Francis atafanya ziara ya kitume katika nchi hii kuanzia Machi 5 hadi 8, 2021, ambapo atazuru mji wa Baghdad, eneo la Ur, jiji la Erbil, pamoja na Mosul na Qaraqosh katika Bonde la Ninawi, "msemaji wa Vatican amesema katika taarifa.

Ziara hii ya kipekee ya papa "inaashiria ujumbe wa amani kwa Iraq na kwa ukanda mzima," wizara ya mambo ya nje ya Iraq imesema katika taarifa.

Kabla ya janga la Corona, Papa Francis alikuwa ameelezea wazi nia yake yake ya kutembelea nchi hii, ambapo amekuwa akibaini kwamba watu wengi "waliouawa" kwa vita nchini humo.

Akipokea wawakilishi wa huduma za misaada kwa Makanisa ya Mashariki mwezi Juni 2019, papa Francis alielezea 'nia' yake ya kuzuru nchi ya Iraq mnamo mwaka 2020. Mwezi Januari 2020 Papa Francis alimpokea huko Vatican rais wa Iraq Barham Salih.