UINGEREZA-CHANJO-AFYA

Covid-19: Matumizi ya chanjo ya Pfizer/BioNTech yaanza nchini Uingereza

Margaret Keenan mwenye umri wa miaka 90, aliyekuwa wa kwanza kupata chanjo ya Covid 19 nchini Uingereza (08/12/2020)
Margaret Keenan mwenye umri wa miaka 90, aliyekuwa wa kwanza kupata chanjo ya Covid 19 nchini Uingereza (08/12/2020) Jacob King/AP

Uingereza imeanza matumizi ya chanjo ya Pfizer / BioNTech kwa watu walio katika mazingira magumu zaidi leo Jumanne asubuhi, na kuwa nchi ya kwanza ya Magharibi kutoa mpango mkubwa wa chanjo dhidi ya virusi vya Corona, vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti.

Matangazo ya kibiashara

Margaret Keenan, 90, ambaye amelazwa hospitalini huko Coventry (katikati mwa Uingereza) alikua mgonjwa wa kwanza ulimwenguni kupokea chanjo hiyo iliyotengenezwa na muungano wa maabara kutoka Marekani na Ujerumani, karibu wiki moja baada ya kutolewa idhini ya kusafirishwa chanjo hiyo katika nchi zilizoathirika zaidi na virusi vya Corona barani Ulaya ambapo watu karibu 61,500 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo hatari wa COVID-19.

Chanjo iliyotengenezwa kwa ushirikiano kati ya kampuni za Pfizer kutoka Marekani na BioNTech ya Ujerumani, imekuwa ya kwanza kuidhinishwa kutumika dhidi ya ugonjwa wa COVID-19, baada ya kukamilishwa hatua za majaribio.

Hivi karibuni kampuni hizo zilisema mamalaka ya udhibiti wa madawa ya nchini Uingereza imewapa idhini ya matumizi ya dharura ya chanjo hiyo. Kampuni hizo tayari zimesaini makubaliano ya kutuma chanjo zipatazo milioni 40 nchini Uingereza katika kipindi cha kati ya mwaka 2020 na 2021.

Uingereza ni nchi ya kwanza duniani kuidhinisha chanjo hiyo ya Pfizer/BioNTech ya kupambana na virusi vya Corona kwa matumizi ya watu wengi. Mamlaka ya Uingereza ya kudhibiti madawa na bidhaa za afya MHRA, imesema chanjo hiyo ambayo mtu atahitaji kudungwa mara mbili tofauti kila baada ya siku 21, inaweza kutoa ulinzi kwa asilimia 95 dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.