UJERUMANI

Covid-19: Biashara zisizo za lazima, shule, kufungwa nchini Ujerumani

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel. Fabrizio Bensch/pool photo via AP

Biashara zote ambazo sio muhimu, pamoja na shule na vitalu vitafungwa nchini Ujerumani kuanzia Jumatano Desemba 16 hadi Januari 10, 2021, Kansela Angela Merkel ametangaza Jumapili, katika jaribio la kuzuia mlipuko wa pili wa virusi vya Corona.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya kubainika 'vifo vingi' kutokana na janga la COVIDI-19 na "kuongezeka kwa visa vingi" vya maambukizi, kiongozi huyo wa kihafidhina, aliyenukuliwa na shirika la habari la AFP, amesema: "tunalazimika kuchukua hatua na tunaanza kuzitekeleza sasa".

Jana Jumapili viongozi wa serikali za majimbo walikutana na kansela Merkel na walikubaliana kimsingi kwamba shule zote zitafungwa katika kipindi chote hicho na waajiri watatakiwa kufunga shughuli zao au kukubali wafanyakazi wafanyie kati majumbani.

Uuzaji wa fataki zinazotumiwa wakati wa kipindi cha mwaka mpya umepigwa marufuku. Kiwango cha maambukizi nchini Ujerumani kila siku pamoja na vifo imefikia rekodi ya juu katika siku za karibuni na wanasiasa wengi wamekuwa wakitoa tahadhari.

Majadiliano ya leo yatafanyika wakati maafisa wa ngazi ya juu nchini Ujerumani wanatoa wito wa kutangazwa marufuku kali zaidi kudhibiti kuenea virusi vya Corona pamoja na rikodi ya juu ya maambukizi inayotia wasiwasi.

Taasisi ya kudhibiti magonjwa nchini Ujerumani ya Robert Koch ilirekodi visa vipya 28,438 katika muda saa 24 zilizopita pamoja na vifo 496 kutokana na COVID-19 idadi ambayo ni kubwa kuwahi kushudiwa nchini humu.

Ujerumani ambayo wakati wa msimu wa machipuko ilikuwa na kiwango kidogo cha vifo ikilinganishwa na mataifa mengine jirani hivi sasa imefikisha idadi ya vifo 21,466 pamoja na maambukizi milioni 1.3 ya virusi vya Corona.