Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, aambukizwa Covid 19
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amethibitishwa kupata maambukizi ya Civid 19, tangazo ambalo linafanya pia maofisa kadhaa wa ikulu ya Paris, kujitenga nyumbani.
Imechapishwa:
Macron anakuwa kiongozi mwingine wa juu duniani kuambukizwa virusi hivyo, akiwemo waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson na rais wa Marekani, Donald Trump.
Ofisi yake imesema Macron, alipimwa baada ya kuanza kuonesha dalili za awali za maambukizi ya Covid na sasa amelazimika kujitenga.
Taarifa ya ikulu imeongeza kuwa ''Rais ataendelea kufanya kazi akiwa amejitenga".
Maambukizi haya anayapata katika wakati mgumu, wakati huu akijaribu kuongoza kampeni ya kuhamasisha raia kujikinga taifa hilo likielekea msimu wa sikukuu.
Rais Macron, alihudhuria kikao cha wakuu wa nchi za Ulaya jijini Brussels, Ubelgiji juma lililopita na haijafahamika ni wapi hasa alipata maambukizi hayo.
Rais wa baraza la Ulaya, Charles Michel, ambaye alihudhuria mkutano wa pamoja na rais Macron, nae ametangaza kujitenga.
Ofisi ya waziri mkuu wa Hispania, Pedro Sanchez, nayo imetangaza kiongozi huyo kwenda kujitenga kwa kuwa alitangamana na raizs Macron.
Kwa matokeo haya ni wazi sasa safari ya rais Macron aliyokuwa amepanga kuifanya juma lijalo nchini Lebanon, ambako amekuwa akishiriki moja kwa moja kusaka suluhu ya kisiasa kwenye taifa hilo, imefutwa.
Taarifa zaidi zinasema waziri mkuu Jean Castex, ambaye nae alitangamana na rais Macron, ameanza kujitenga.