UINGEREZA

COVID-19: Baadhi ya maeneo ya jiji la London yawekewa masharti mapya

Soko la  Broadway jijini London nchini Uingereza
Soko la Broadway jijini London nchini Uingereza REUTERS/Henry Nicholls

Kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona, mamilioni ya watu wanaoishi katika mikoa kadhaa iliyoko mashariki na Kusini-Mashariki mwa Uingereza watakuwa chini ya masharti mpya kuanzia siku ya Jumamosi.  

Matangazo ya kibiashara

Kuanzia siku ya  Jumamosi watu milioni 38, sawa na asilimia  68% ya raia wa Uingereza, wako katika maeneo yaliyo chini ya kiwango ambacho kina tahadhari kubwa ya maambukizi.

Miongoni mwa masharti yanayozingatiwa katika eneo hilo ni pamoja na  kufungwa kwa baa, mikahawa, hoteli, majumba ya kumbukumbu na kumbi za sherehe na matukio.

Mji mkuu London, ambao umeathirika sana na mlipuko wa pili wa COVID-19, umewekwa katika kiwango cha juu cha vizuizi siku ya Jumatano.

Waziri wa Afya Matt Hancock ameelezea wasiwasi kufuatia kuongezeka kwa 46% ya maambukizi katika wiki iliyopita Kusini Mashariki na theluthi mbili mashariki mwa Uingereza.

Hata hivyo Waziri Mkuu wa Uingereza anakabiliwa na shinikizo kubwa kufuata majimbo mengine ya nchi hiyo: Ireland Kaskazini imetangaza kwa mara ya tatu masharti mapya ya watu kutotembea kuanzia Desemba 26 kwa wiki sita, wakati jimbo la Wales limetangaza masharti kama hayo ambayo yataanza kutekelezwa kuanzia Desemba 28 kwa kipindi kisichojulikana.