UFARANSA

Acat-France na RSF zataka ukweli kuhusu kifo cha mwanahabari Samuel Wazizi

Shirika la wanahabari wasio na mipaka RSF lashinikiza ukweli kuhusu vifo vya wanahabari
Shirika la wanahabari wasio na mipaka RSF lashinikiza ukweli kuhusu vifo vya wanahabari AFP/Bertrand Guay

Shirika linalotetea haki za binadamu nchini Ufaransa, Acat-France na Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka RSF limeiomba mamlaka nchini Ufaransa kutoa taarifa kuhusu kifo cha mwandishi wa habari Samuel Wazizi aliyefariki akiwa kizuizini mwaka 2019.

Matangazo ya kibiashara

Mamlaka nchini Cameroon inakanusha kuhusika na kitendo chochote cha mateso ambacho wengi wanaona kuwa kilisababisha kifo cha mwandishi huyo.

 

"Matokeo ya uchunguzi kuhusu kifo cha mwandishi wa habari wa Cameroon Samuel Wazizi ambaye alifariki dunia akiwa kizuizini yanapaswa kuwekwa wazi. Hiki ni kilio cha kutoka mashirika mawili ya haki za binadamu Acat-France na RSF.

 

Samuel Wazizi alikamatwa katika mji wa Buea, Kusini Magharibi mwa Cameroon Agosti 2, 2019.

Ilichukua miezi kumi kwa mamlaka ya Cameroon, baada ya vyombo vya habari vya kitaifa kuweka wazi kifo chake, kukubali kwamba mwandishi huyo wa habari alifariki dunia.

 

Taarifa ya wizara ya Ulinzi ilibainisha kuwa baada ya kukamatwa Agosti 2 huko Ekona, Kusini-magharibi mwa nchi, Samuel Wazizi ambaye jeshi lilimtaja kama "mweka hazina wa makundi mbali mbali ya kigaidi" alikuwa amepelekwa kuhojiwa na idara husika huko Yaoundé.

Hata hivyo alipokelewa kwenye idara hiyo akiwa katika hali mbaya ya kiafya na hivyo kupelekwa hospitalini mara moja. Lakini alifariki dunia siku chache baadaye, Agosti 17, 2019 , kutokana na mchtuko wa moyo.

Hajafanyiwa kitendo chochote kile cha kikatili au mateso ya aina yoyote, alibaini mkuu wa kitengo cha mawasiliano katika Wizara ya Ulinzi.

 

Chama cha waandishi wa habari nchini Cameroon, SNJC, na Chama cha waandishi wa habari kutoka maeneo yanayozungumza Kiingereza nchini humo yalifutilia mbali maelezo hayo ya Wizara ya Ulinzi, na kusema kuwa ni uongo mtupu.