EU-UK

Brexit: London yabainisha msimamo wake kuhusu kujitoa EU

Waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson
Waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson REUTERS/Toby Melville/Pool

Uingereza itamaliza kipindi cha mpito kilichofuata mchakato wa nchi hiyo kuondoka katika Umoja wa Ulaya mnamo Desemba 31, msemaji wa Waziri Mkuu Boris Johnson amethibitisha leo Jumatatu.

Matangazo ya kibiashara

Waziri Mkuu wa Scotland Nicola Sturgeon hapo awali alitaka kuongezewa muda wa kipindi hiki kwa sababu ya matatizo yanayotokana na ugunduzi wa aina mpya ya mlipuko wa virusi vya Corona.

 

"Msimamo wetu juu ya kipindi cha mpito uko wazi [...] kipindi hiki kitamalizika Desemba 31, huu ndio bado msimamo wetu," msemaji wa Waziri Mkuu Boris Johnson amewaambia waandishi wa habari.

 

"Tunapaswa kuidhinishe makubaliano yoyote kabla ya Januari 1, hii inamaanisha kuwa wakati unakwisha na ndio sababu wajumbe wetu katika mazungumzo wanaendelea kufanya kazi kwa bidii," ameongeza.

 

Kiongozi wa Umoja wa Ulaya anayeratibu mazungumzo ya Brexit, Michel Barnier na mwenzake wa Uingereza David Frost, walikutana Brussels jana, lakini masuala muhimu yalishindwa kutatuliwa.

Bunge la Ulaya limesema mazungumzo hayo yalipaswa kukamilika jana, ili kuridhia makubaliano ifikapo Desemba, 31.

 

Duru kutoka kwa afisa wa ngazi ya juu wa Uingereza zimeeleza kuwa bado kuna tofauti kubwa kwenye mazungumzo hayo na makubaliano hayatofikiwa hadi hapo patakapokuwa na mabadiliko makubwa kutoka Brussels.

 

Muda wa mazungumzo hayo umekwisha na Uingereza inatarajiwa kuondoka kwenye soko la pamoja la Umoja wa Ulaya chini ya wiki mbili, lakini pande zote mbili zinatarajia mazungumzo yataendelea kwa siku tatu au nne.