CANADA-UK

Canada yasitisha safari za ndege kuelekea Uingereza

Nchi ya Canada ni miongoni mwa mataifa yaliyositisha safari za ndege na Uingereza.
Nchi ya Canada ni miongoni mwa mataifa yaliyositisha safari za ndege na Uingereza. Graham Hughes/The Canadian Press via AP

Canada imetangaza kusitisha safari za ndege kuelekea Uingereza, baada ya taifa hilo kushuhudia ongezeko kubwa la maambukizi ya COVID-19

Matangazo ya kibiashara

Katika barua iliyotumwa kwa marubani, wizara ya uchukuzi ya Canada iimebaini kwamba hatua hii ni "muhimu kwa usalama wa anga na ulinzi wa umma"

Hatua hii haitumiki kwa ndege za mizigo, wizara ya uchukuzi ya Canada imeongeza katika taarifa.

Maafisa kadhaa wa Canada, pamoja na Waziri Mkuu Justin Trudeau, walikutana Jumapili alasiri kujadili mikakati mpya ya kudhibiti janga la COVID-19, Waziri wa Afya Patty Hadju amesema kupitia Twitter.

Canada inafuata nyayo za Ufaransa na nchi kadhaa za Ulaya ambazo zilitangaza saa chache mapema Jumapili kusitisha safari zote za ndege kuelekea Uingereza.

Jijini London, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, ambaye alitangaza hatua kali za kiafya siku ya Jumamosi, anatarajia kufanya mkutano wa dharura Jumatatu kujadili maswala ya kimataifa ya uchukuzi.

Idadi ya visa vya maambukizi vinaendelea kuongezeka nchini Canada, ambapo kampeni ya chanjo ilianza wiki iliyopita. Karibu visa 507,800 vya maambukizi vimeripotiwa nchini humo, ikiwa ni pamoja na zaidi ya visa 6,200 Jumapili pekee.

Kulingana na vyombo vya habari nchini Canada, jimbo lenye idadi kubwa ya watu nchini, Ontario, litaanza kutekeleza hatua ya watu kutotembea kuanzia Desemba 24.