UINGEREZA

Boris Johnson: Ninaelewa hatua ya mataifa ya kigeni dhidi ya Uingereza

Waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson
Waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson Toby Melville/Pool Photo via AP

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, amesema anaelewa hatua ya mataifa ya kigeni kusitisha safari zake za ndege nchini humo kutokana na nchi hiyo kushuhudia kuenea kwa haraka kwa aina mpya ya virus vya Corona.

Matangazo ya kibiashara

Mataifa zaidi ya 40 yamesitisha safari za ndege kati yao na Uingereza, wakati huu viongozi wa Umoja wa Ulaya wakitarajiwa kuja na mkakati mmoja wa kupambana na janga hili.

 

Nchi zilizojiunga na orodha na mataifa kadhaa ya Ulaya ni pamoja na Kuwait, Tunisia, Urusi, Oman, Saudi Arabia pamoja na Chile. Nchi nyingine ni Israel, El Salvador, Morocco, India, Jordan na Argentina. Mbali na Uingereza, nchi hizo zimezuia pia ndege kutoka na kwenda Afrika Kusini na Denmark, ambako kuna virusi vipya vilivyogundulika

 

Waziri wa Usafiri wa Ufaransa, Jean-Baptiste Djebbari, amesema maafisa wanatarajia kuanzisha hatua za usafi barani Ulaya katika muda wa saa chache zijazo ambazo zitaruhusu usafiri kutoka Uingereza kuanza tena.

 

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema kwamba vizuizi vya usafiri vimewekwa katika juhudi za kuepusha hali ya kutodhibitika kwa virusi hivyo, lakini hilo sasa linaratibiwa na nchi wanachama 27 za Umoja wa Ulaya.

 

Wakati huo huo Shrika la Afya Duniani, WHO, limetahadharisha dhidi ya wasiwasi wa kupindukia kuhusu aina mpya ya virusi vya Corona vinavyosamba kwa kasi kubwa, baada ya kugunduliwa nchini Uingereza na baadae Afrika Kusini.

 

Maafisa wa WHO wamesema hawana ushahidi wowote unaoonyesha kwamba aina hiyo mpya ya virusi inawafanya watu kuwa wagonjwa zaidi au kuwa ni mbaya zaidi kuliko virusi vilivyokuwepo awali vya ugonjwa wa COVID-19. Ingawa WHO imethibitisha kwamba aina hiyo mpya inaonekana kuenea kwa kasi zaidi.

 

Uingereza ina mamabukizi zaidi ya Milioni mbili, huku watu wengine zaidi ya Elfu 67 wakipoteza maisha.