UJERUMANI

Covid 19: Visa zaidi ya 32,000 na vifo vipya 800 vyathibitishwa nchini Ujerumani

Virusi vya Corona
Virusi vya Corona NIAID-RML via AP

Idadi ya visa vilivyothibitishwa vya maambukizi ya virusi vya Corona nchini Ujerumani imepanda hadi 1,587,115, baada ya visa vipya 32,195 kuthibitishwa siku moja iliyopita, kulingana na takwimu zilizotolewa leo Alhamisi na kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa cha Robert Koch (RKI).

Matangazo ya kibiashara

Kituo hiki pia kimeripoti vifo vipya 802, na kufikisha jumla ya vifo 28,770 tangu kuzuka kwa janga hilo nchini Ujerumani.

Hayo yanajiri wakati mataifa kadhaa ya Ulaya jana Jumatano yalianza kulegeza marufuku ya safari yaliyokuwa yameiwekea Uingereza katika juhudi za kukabiliana na kuenea kwa aina mpya ya kirusi cha Corona wakati maafisa wa Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO wakitazamiwa kulijadili suala hilo.

Umoja wa Ulaya umeyataka mataifa ya bara hilo kuacha kuchukua hatua ya kufunga mipaka ya nchi zao.

Ufaransa imeanza kuifungua mipaka yake na Uingereza tanguJumatano, ingawa vipimo kwa ajili ya COVID-19 vitahitajika. Uholanzi nayo imetangaza kuondoa marufuku hiyo, lakini sio kwa abiria wote.

Kirusi kipya cha Corona kimeikumba Uingereza na kuibua wasiwasi duniani kote wakati chanjo ya COVID-19 ikianza kutolewa.