UINGEREZA-EU

Uingereza na Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, akiwa na rais wa Tume ya Umoja Ulaya Ursula von der Leyen, katika siku za hivi karibuni.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, akiwa na rais wa Tume ya Umoja Ulaya Ursula von der Leyen, katika siku za hivi karibuni. Daniel LEAL-OLIVAS / AFP

Uingereza na Umoja wa Ulaya, zimekubaliana kuhusu namna ya kufanya biashara baada ya London kuondoka kwenye Umoja huo ifikapo mwisho wa mwaka 2020.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja baada ya msururu wa mazungumzo ya miezi kadhaa kati ya wawakilishi wa Uingereza na wale wa Umoja wa Ulaya, jijini Brussels nchini Ubelgiji.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, amesema kuwa mkataba huo unaridhisha na ni wa kihistoria.

“Mkataba huu ni mafanikio makubwa sana kwetu kwa sababu tumechukua tena udhibiti wa sheria zetu, mipaka yetu na haki yetu ya uvuvi,” amesema Boris kwenye hotuba kwa taifa lake.

Baada ya taarifa ya kupatikana kwa mkataba huo, wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya siku ya Ijumaa wanatarajiwa kupewa taarifa ya kina kuhusu kilichokubaliwa kwenye mkataba huo.

Wabunge nchini Uingereza nao pia wanasubiri mkataba huo kabla ya kuujadili na kuupigia kura tarehe 30 Disemba ili uanze kutekelezwa.

Chama cha upinzani cha Labour, licha ya kutofurahishwa na mkataba huo, kinatarajiwa kuunga mkono kwa kile viongozi wa chama hicho wanasema, unashinda kukosa mkataba kabisa.

Nao wabunge wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuujadili mswada huo mapema mwaka 2021.