UJERUMANI

Coronavirus: Zaidi ya visa vipya 14,400 vyaripotiwa nchini Ujerumani

Ujerumani yarekodi maambukizi zaidi ya Covid 19 wakati huu nchi za Ulaya zikianza kutoa chanjo kwa raia.
Ujerumani yarekodi maambukizi zaidi ya Covid 19 wakati huu nchi za Ulaya zikianza kutoa chanjo kwa raia. JOEL SAGET / AFP

Idadi ya visa vilivyothibitishwa vya maambukizi ya virusi vya Corona  nchini Ujerumani imepanda hadi 1,627,103, baada ya visa 14,455 kuthibitishwa siku moja iliyopita, kulingana na takwimu zilizotolewa na kituo cha kuzuia na kudhibiti magonjwa cha Robert Koch (RKI).

Matangazo ya kibiashara

Taasisi hiyo pia imeripoti vifo vipya 240, na kufikisha jumla ya vifo 29,422 tangu kuzuka kwa janga hilo nchini Ujerumani.

Hayo yanajiri wakati zoezi la utoaji chanjo ya virusi vya Corona lilianza rasmi Jumamosi katika majimbo 16 ya Ujerumani. Watu wa kwanza kupatiwa chanjo walikuwa ni wale walio na umri wa zaidi ya miaka 80, wauguzi na wafanyakazi wa hospitali ambao wako katika hatari kubwa ya maambukizi ya virusi hivyo.

Serikali imewahimiza wananchi kupewa chanjo kwa manufaa yao na kuwalinda wengine. Wataalamu wamesema kiwango cha asilimia 60 hadi 70 cha chanjo ni muhimu ili kuweza kudhibiti kirusi hicho.

Nchi nyingi za Umoja wa Ulaya zilianza rasmi zoezi hilo jana Jumamosi, wakati aina mpya kirusi kinachosambaa kwa kasi kikiripotiwa katika mataifa ya Ulaya.

Hata hivyo Shirika la Afya Duniani, WHO, linaonya kwamba janga hilo la sasa halitakuwa la mwisho na kwamba ni muda wa kujifunza kutoka janga la virusi vya Corona.