UJERUMANI

Coronavirus: Zaidi ya visa vipya 32,500 vyarekodiwa nchini Ujerumani

Maabara ya nchini Ujerumani.
Maabara ya nchini Ujerumani. Marijan Murat / dpa / AFP

Idadi ya visa vilivyothibitishwa vya maambukizi ya virusi vya Corona nchini Ujerumani vimepanda hadi 1,719,737, baada ya visa vipya 32,552 kuthibitishwa siku moja iliyopita, kulingana na takwimu zilizotolewa leo Alhamisi na kiuto cha kuzuia na kudhibiti magonjwa cha Robert Koch.

Matangazo ya kibiashara

Taasisi hiyo pia imeripoti vifo vipya 964, na kufikisha jumla ya vifo 33,071 tangu kuzuka kwa janga hilo nchini Ujrumani.

Hayo yanajiri wakati maafisa nchini Ujerumani waliweka bayana Jumatanu wiki hii kwamba vizuizi vya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona havitalegezwa mwanzoni mwa mwezi Januari.

Ujerumani tayari imeweka masharti kadhaa ya kudhibiti janga la COVID-19, ikiwa ni pamoja na kufunga shule na maduka, kuhimiza watu kuvaa barakoa, watu kutosogeleana na marufuku kwa mikusanyiko.Masharti hayo yanapaswa kudumu hadi Januari 10.

Kansela Angela Merkel na mawaziri wakuu wa majimbo 16 wanatarajiwa kukutana Jumanne wiki ijayo kutathmini hatua zaidi.

Wakati huo huo huo Bi Merkel katika hotuba yake mwaka mpya kwa Ujerumani, amewashambulia wale wanaopinga uwepo wa virusi vya corona, huku akikiri kwamba mwaka mzima wa 2020 ndio umekuwa mwaka wenye changamoto chungunzima katika uongozi wake wa miaka 15.

Kansela Merkel amewapongeza wahudumu wa afya katika kupambana na janga hili pia na wafanyakazi wengine waliokuwa muhimu mwaka 2020.

Kufikia sasa Wajerumani milioni 1.7 wameambukizwa virusi vya Corona na wengine 32,000 kufariki dunia.

Idadi ya visa vya maambukizi na vifo inazidi kungezeka. Siku ya Jumatano pekee zaidi ya watu elfu moja walifariki katika kipindi cha saa ishirini na nne, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuzuka kwa janga COVID-19 nchini Ujerumani.