UINGEREZA-MAREKANI

Mahakama nchini Uingereza yakataa kumkabidhi Julian Assange nchini Marekani

Wafuasi wa Julian Assange, wakiwa nje ya Mahakama jijini London
Wafuasi wa Julian Assange, wakiwa nje ya Mahakama jijini London REUTERS/Peter Nicholls

Mahakama jijini London nchini Uingereza, imeamua kuwa, Julian Assange mwanzilishi wa mtandao wa kiuchunguzi wa Wikileaks, hawezi kusafirishwa nchini Marekani kufunguliwa mashtaka.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Vanessa Baraitser, akisema Assange, raia wa Australia hawezi kusafirishwa nchini Marekani kwa sababu ya afya yake ya akili na huenda akajiua iwapo atakwenda nchini Marekani.

Assange mwenye umri wa miaka 49 anatakiwa nchini Marekani baada ya mwaka 2010 na 2011 kuchapisha maelfu ya taarifa za siri za Marekani katika matandao wake, hatua ambayo Marekani inasema ilikuwa kinyume cha sheria na kuhatarisha usalama wa watu.

Baada ya uamuzi huu, Marekani ina siku 14 kukataa rufaa. Assange mwenyewe amekuwa akisema mashtaka dhidi yake nchini Marekani, yamechochewa kisiasa.

Kwa sasa Assange anazuiwa gerezani akisubiri ombi la kuachuliwa kwa dhamana na wakili wake amesema mteja wake hawezi kutoroka.

Assange ambaye amekuwa nchini Uingereza tangu mwaka 2012 na wakati mmoja kupewa hifadhi katika ubalozi wa Ecuador, alikuwa Mahakamani na wakati Jaji akisoma uamuzi dhidi yake, alionekana akifumba macho.