IRAN-SIASA

Iran yaishutumu Marekani kwa kuingilia masuala ya ndani ya taifa hilo

Rais mteule wa Iran Ebrahim Raisi akiwapungia wafuasi wake baada ya kutangazwa mshindi kwenye mji wa Teherán, Juni 18 2021
Rais mteule wa Iran Ebrahim Raisi akiwapungia wafuasi wake baada ya kutangazwa mshindi kwenye mji wa Teherán, Juni 18 2021 ATTA KENARE AFP

Nchi ya Iran, imelaani vikali matamshi ya serikali ya Marekani, kuhusu uchaguzi wake wa juma lililopita, utawala wa Tehran, ukisema matamshi yake yanaingilia masuala ya ndani ya taifa hilo.

Matangazo ya kibiashara

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani, ilisema mwishoni mwa juma lililopita kuwa, uchaguzi wa Iran haukuwa huru wala wa haki.

Kauli ya Tehrani, imekuja siku moja tu tangu kiongozi mpya wa taifa hilo, Ebrahim Raisi, azungumze na kuikashifu Marekani, huku akisema mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia lazima uwe kwa maslahi ya raia na si vinginevyo.

Ebrahim Raisi amesema kuwa anaunga mkono mazungumzo kati ya Iran na madola sita yenye nguvu ya kuufufua muafaka wa nyuklia wa 2015 lakini akapinga wazi wazi kukutana na Rais wa Marekani Joe Biden, hata kama Marekani itaondoa vikwazo vyote ilivyoiwekea nchi hiyo.

Aidha Raisi, amesema kwa sasa hana nia ya kukutana kwa mazungumzo na rais wa Marekani, Joe Biden.

Raisi, mwenye umri wa miaka 60, na ambaye ni mkosoaji mkali wa nchi za Magharibi, atachukua usukani kutoka kwa Hassan Rouhani mnamo Agosti 3 wakati Iran ikilenga kuuokoa mkataba unaoyumba wa nyuklia na iondolewe vikwazo vikali vya Marekani ambavyo vimeuharibu uchumi wa nchi hiyo.