TANZANIA -FASIHI

Wasomi wajadili nafasi ya fasihi Afrika

Pierre Astier na Walter Bgoya wakizungumza kuhusu fasihi na uchapishaji katika ubalozi wa Ufaransa Tanzania. 16 Novemba 2017
Pierre Astier na Walter Bgoya wakizungumza kuhusu fasihi na uchapishaji katika ubalozi wa Ufaransa Tanzania. 16 Novemba 2017 RFI/Emmanuel Makundi

Kukua kwa lugha ndogondogo na maendeleo ya teknolojia kunaelezwa kuchangia pakubwa kuimarika na kukua kwa waandishi wa fasihi na wachapishaji barani Afrika, licha ya changamoto za kifedha ambazo zinawakabili waandishi.

Matangazo ya kibiashara

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mazungumzo kuhusu changamoto na fursa za uandishi na uchapishaji barani Afrika na Ulaya, muandishi na muasisi wa shirika la Agence Literaire la Ufaransa Pierre Astier na mchapishaji maarufu nchini Tanzania Walter Bgoya, wanasema tasnia ya uandishi wa vitabu bado inakabiliwa na changamoto nyingi barani Afrika.

Akichangia kwenye mazungumzo hayo yalioandaliwa na balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Malika Berak, Walter Bgoya amesema kwa nchi nyingi za Afrika suala la uandishi wa fasihi bado ni changamoto kutokana na ukweli kuwa hata wasomaji wa vitabu hakuna wakutosha akitolea mfano nchini Tanzania.

“Mfano nchini Tanzania kuna watu zaidi ya milioni 40 lakini waandishi unaweza kuta wako asilimia 2 tu ya watanzania wote, hii ni changamoto kwa kuwa hata wakichapisha vitabu vingi bado wanunuzi ni wachache na niwatu wa kipato cha kati”. Alisema Bgoya.

Bgoya ameongeza kuwa suala la soko pia kwa Tanzania ni changamoto kwa kile alichosema kuna wakati hata yeye kama mchapishaji nalazimika kuzikataa kazi za baadhi ya waandishi kwa kukosa ustadi wa kiuandishi.

Kwa upande wake Pierre Astier amekiri hivi sasa kuna changamoto zinazofanana kidunia, akitolea mfano mashirika makubwa ya uchapishaji ambayo baadhi yao yamepigwa marufuku kufanya kazi kwenye baadhi ya nchi.

Astier amesema kuwa suala la lugha ni changamoto nyingine inayoikabili fasihi, akisema lugha mbili kubwa za Kifaransa na Kiingereza ndizo lugha zinazozungumzwa na kuandikwa sana na waandishi ukilinganisha na lugha nyingine.

“Mfano nchini Marekani raia wake wengi wanazungumza lugha moja tu ya Kiingereza kwahivyo wanalazimika kusoma vitabu vilivyoandikwa kwa Kiingereza au kutafsiriwa, hii ni changamoto katika ukuaji wa fasihi na hata kwa wachapishaji”. Alisema Astier.

Hata hivyo wataalamu wote wawili walikubaliana kuwa kuna soko la fasihi kidunia na kwamba ni lazima Serikali za dunia ziruhusu kuwa na wachapishaji binafsi ili kuongeza ushindani kwa kuwa tasnia hii ikitumika vizuri inaweza kukuza uchumi wa waandishi, wachapishaji na Serikali.

Kwa upande wake balozi Berak ambaye hivi karibuni anaelekea kumaliza muda wake nchini Tanzania, amesema anajivunia kuona namna ambavyo mpango wa ushirikiano wa kiuchumi na kitamaduni aliouanzisha kati ya Tanzania na Ufaransa umeendelea kupata mafanikio.

“Najivunia mafanikio haya na kumbe hiki kimekuwa ni kitu kizuri cha ushirikiano na kuwaleta pamoja watu wa Tanzania na Ufaransa”. Alisema Berak.

Ijumaa ya wiki hii ubalozi wa Ufaransa uliandaa mjadala mwingine kuhusu fasihi na uchapishaji katika kituo chake cha utamaduni cha Alliance Francaise, ambapo waandishi na wachapishaji watajadiliana kuhusu mchango wa fasihi kwenye jamii zetu.

Wanadiplomasia, wasomi na wanataaluma wa fasihi wa kimataifa wakiwa nchini Tanzania wamezungumzia nafasi ya tasnia hiyo kuwa ina umuhimu mkubwa katika shughuli za maendeleo.

Wakizungumza wakati wa kongamano la fasihi lililoandaliwa na kituo cha Alliance Francaise Jijini Dar es Salaam wasomi hao wamesema fasihi imeleta maendeleo kwenye nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa endapo itatiliwa mkazo katika matumizi yake.

Mkuu wa kitengo cha Ushirikiano na Utamaduni katika Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Prosefa Philippe Boncour amezipa changamoto nchi za Afrika kuthamini fasihi kwa kuzingatia umuhimu wake katika maendeleo.

“Kiswahili mathalani ni bidhaa yenye watumiaji zaidi ya milioni 100. Ni muhimu watunzi na wanafani kuongeza ubunifu ili kupata soko la bidhaa zao kama vitabu na ushairi”.

Mhadhi wa idara ya fasihi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dr Rose Mbijima amesema ipo haja kwa serikali na sekta binafsi kuongeza ushirikiano ili kuongeza idadi ya wasomi na wazalishaji wa kazi za fasihi.

Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Malika Berak na maofisa kutoka balozi mbalimbali zilizopo nchini Tanzania.