TANZANIA-SANAA

Diamond ajikuta matatani kwa kusambaza picha chafu mitandaoni

Msanii nyota katika muziki wa kizazi kipya maarufu Bongo Fleva nchini Tanzania Nassib Abdul Juma maarufu Diamond Platnumz alikamatwa na polisi siku ya Jumatatu wiki hii na alihojiwa kutokana na kusambaza picha chafu mtandaoni.

Nassib Abdul Juma, nyota wa Tanzania maarufu Diamond Platnumz, alikamatwa Jumatatu, Aprili 17, 2018 Dar es Salaam.
Nassib Abdul Juma, nyota wa Tanzania maarufu Diamond Platnumz, alikamatwa Jumatatu, Aprili 17, 2018 Dar es Salaam.  Naseeb Abdul Juma
Matangazo ya kibiashara

Video hiyo ilisambazwa kwenye kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii ikimuonyesha akiwa kitandani akicheza na mzazi mwenzake Hamisa Mobetto pia na mwanamke mwingine ambaye hajajulikana, picha zinazoelezwa kuwa hazina maadili.

Waziri wa Habari, Harrison Mwakyembe, amesema msanii Diamond Platnumz alikamatwa siku ya Jumatatu wiki hii kwa makosa ya kusambaza picha zilizokosa maadili mitandaoni na sasa anahojiwa na polisi.

Akizungumza bungeni leo Aprili 17, Waziri Mwakyembe amesema serikali imeshatunga sheria inayowabana wasanii na kudhibiti maudhui yasiyo na maadili mitandaoni.

Mbali na hilo Mwakyembe ameagiza msanii mwingine Nandi kusakwa na polisi akisisitiza kauli yake kuwa Tanzania siyo kokoro la uchafu.

Ametoa kauli hiyo wakati anajibu swali la nyongeza la mbunge wa Ulanga Godluck Mlinga aliyetaka kujua serikali ina mkakati gani kukomesha tabia za baadhi ya watu wanaotumia mitandao vibaya ikiwemo kuhamasisha masuala ya ushoga.

Awali serikali ilitaja changamoto kubwa inayolikabili taifa ni athari ya utamaduni wa nje katika maadili, mila na desturi za Mtanzania kutokana na kuwepo na muingiliano mkubwa wa watu duniani.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Juliana Shonza wakati akijibu swali la mbunge, Nuru Awadh Bafadhili.

Mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanasimamia maadili.

Hata hivyo Shonza amesema kinacholeta shida hadi nyimbo kuwa hazina maadili ni tabia ya wasanii kutopeleka nyimbo zao kuhaririwa katika baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)

Iwapo watafikishwa mahakamani, wawili hao wanaweza kushtakiwa chini ya kifungu cha Sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 ambayo inakataza kuweka kwenye mfumo wa kompyuta au taarifa nyingine yeyote kwenye mfumo wa mawasiliano picha mbaya, kama vile picha chafu za ngono.