VATICAN-KANISA-KASHFA YA NGONO

Vatican kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji kwa watoto

Papa Francis katika eneo la St Peter (picha ya kumbukumbu).
Papa Francis katika eneo la St Peter (picha ya kumbukumbu). REUTERS/Osservatore Romano/Handout

Mkutano wa kipekee juu ya ulinzi wa watoto katika Kanisa Katoliki", mkutano unaosubiriwa na wengi, unafunguliwa leo Alhamisi asubuhi huko Vatican.

Matangazo ya kibiashara

Washiriki 190 kutoka duniani kote wanatarajia kukutana kwa siku tatu jijini Roma. Huu ni mkutano muhimu wa kimataifa kwa Kanisa Katoliki linalokabiliwa na kashfa ya udhalilishaji wa kingono kwa watoto.

Mwishoni mwa majira ya joto, baada ya kufichuliwa kashfa mpya ya viongozi wa kanisa wanaojihusisha na vitendo vya udhalilishaji kwa watoto nchini Marekani, Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Papa Francis na baraza lake la makardinali waliamua kuitisha mkutano wa kimataifa.

Katika mkutano huo watashiriki wakuu 114 wa mabaraza ya maaskofu wa Kanisa Katoliki: 36 kutoka Afrika, 32 kutoka Ulaya, 24 kutoka Amerika na 18 kutoka Asia. Mkutano huu uliandaliwa kabla na kamati ya maandalizi.

Mapema mwezi huu Papa Francis alikiri kuwa makasisi wa Kanisa Katoliki wanawatumia watawa kama watumwa wa ngono.

Inaaminiwa kuwa hii ni mara ya kwanza Papa Francis kukiri hadharani kuhusu dhulma za kingono dhidi ya watawa wa kanisa hilo kubwa zaidi duniani.

Papa alitoa tamko hilo kwa wanahabari akiwa kwenye ziara yake kihistoria katika eneo la mashariki ya kati.

Alikiri kuwa makasisi na maaskofu wamekuwa wakiwanyanyasa watawa, na kwamba kanisa "linashughulikia suala hilo".

Simulizi za unyanyasaji zimekuwa zikijitokeza katika kila kona ulimwenguni. Na kanisa limekuwa likishutumiwa kwa kutetea uhalifu wa makasisi.

Papa Francis pia anapaswa kukabiliana na ukweli uliopo, mitazamo na vitendo ambavyo vinapelekea utamaduni wa unyanyasaji kukua.